
Kundi la mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu limeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutekeleza hati za kukamatwa zilizotolewa dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa masuala ya kijeshi Yoav Gallant, kwa uhalifu wa vita uliofanywa katika vita vya mauaji ya halaiki Gaza.
Mashirika hayo ni pamoja na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Al-Karama ya mjini Geneva, Chama cha Waathirika wa Mateso mjini Geneva, Kituo cha al-Shabaka kwa Haki za Binadamu mjini London, Sauti Huru kwa Haki za Binadamu mjini Paris, Shirika la Kimataifa la EFDD la mjini Ubelgiji, Taasis ya Adalah kwa Haki za Binadamu mjini Istanbul, na Mshikamano kwa Haki za Binadamu mjini Geneva. Tammko hilo la pamoja limetolewa katika Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina ambapo mashirika hayo yametaka hatua hiyo ichukuliwe dhidi ya viongozi wa Israel kwa kuhusika kwao katika maafa makubwa huko Gaza
Mashirika hayo yamesisitiza kuunga mkono hatua za mahakama ya ICC ya The Hague katika kesi dhidi ya Israel, yakitaka utekelezaji wa haraka wa hati za kukamatwa viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa uhalifu wa vita, ikiwemo kutumia njaa kama silaha ya vita, pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu kama vile mauaji ya makusudi, mateso na vitendo vingine vya kinyama.
Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina imewadia wakati Gaza ikikabiliwa na makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano, ambayo hayajamaliza janga la kibinadamu linalowaathiri zaidi ya watu milioni mbili katika eneo hilo.
Mashirika hayo yameonya kuwa mshikamano wa maneno pekee hautoshi tena, ikizingatiwa uendelevu wa ukaliaji wa mabavu wa Israel na sera za ukandamizaji za utawala wa Tel Aviv ambazo ndizo chanzo kikuu cha mateso ya Wapalestina.
Aidha yamesisitiza kuwa mshikamano wa kweli huanza kwa kulaani ukiukaji, kupinga ukwepaji wa adhabu, na kuunga mkono haki ya Wapalestina kujenga dola huru inayojumuisha ardhi yote ya Palestina, huku al-Quds ikiwa mji mkuu wake.
Mashirika hayo yameeleza kuwa hali ya Gaza tangu Oktoba 2023 ni mauaji ya kimbari kamili kwa mujibu wa Mkataba wa Mauaji ya Halaiki wa mwaka 1948, na yakatoa wito wa hatua za haraka na thabiti za kimataifa, yakitaka serikali zote na taasisi za kimataifa zishinikize Israel kuheshimu sheria za kibinadamu za kimataifa, kusitisha mashambulizi dhidi ya raia, na kuruhusu kuingia kwa haraka na bila vizuizi kwa misaada ya kibinadamu na vikosi vya uokozi Gaza.
Tangu Oktoba 2023, jeshi la Israel limekuwa likitekeleza mauaji ya kimbari Gaza na hadi sasa jeshi hilo katili limeua Wapalestina wasiopungua 70,100 — wengi wao wakiwa wanawake na watoto — na kuwajeruhi angalau 170,900 katika vita vya miaka miwili Gaza ambavyo vimegeuza sehemu kubwa ya ukanda wa pwani kuwa magofu.
ICC ilitoa hati za kukamatwa Netanyahu na Gallant mnamo Novemba 21, 2024, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Aidha wawili hao wanaandamwa na mashitaka ya kusababisha, kurefusha au kushajiisha vita vya mauaji ya halaiki vilivyoanza Octoba 2023 huko Gaza, ambavyo hadi sasa vimeua zaidi ya Wapalestina 67,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.