Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imezitaka mahakama za kimataifa na vyombo husika kuwafungulia mashtaka wale waliohusika wa uhalifu wa kivita baada ya uchunguzi kufichua kwamba wanajeshi wa Israel waliteketeza miili ya Wapalestina waliokuwa katika safu za kupokea misaada na kuizika katika makaburi yasiyo na kina huko Gaza.

Harakati hiyo yenye makao yake makuu Gaza, imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) hasa kufuatilia uhalifu huo mbaya, kuujumuisha katika ripoti za uhalifu wa utawala wa Tel Aviv, na kuwafikisha viongozi wa Israel mbele ya sheria kwa uhalifu wao dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Hamas imeeleza kuwa uchunguzi wa CNN, uliopewa jina la “Bulldozed Corpses and Unmarked Graves,” unatoa ushahidi mpya wa moja ya vipengele vya mauaji ya kimbari ya kimfumo ya Israel dhidi ya Wapalestina, na unatoa uthibitisho zaidi wa “jaribio lake la makusudi la kugeuza misaada ya kibinadamu kuwa mitego ya mauaji ya kimbari.”

Harakati hiyo ya mapambano ya ukombozi wa Palestina imesema kwamba uhalifu huo “mbaya” ni sehemu ya uhalifu wa kivita na mashambulizi ya kimfumo, ambayo Israel inayafanya mbele ya macho ya jamii ya kimataifa, kwa kupuuza kabisa sheria ya kimataifa na kanuni za msingi za haki za binadamu.

Taarifa ya Hamas imesema kwamba ukatili huu unafanyika kwa ushirikiano wa utawala wa Marekani na baadhi ya serikali za nchi za Magharibi, sambamba na juhudi za kuzuia mashtaka ya kimataifa dhidi ya wahalifu wa kivita wa Israel, hasa Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu.

Zaidi ya Wapalestina 2,000 wanaripotiwa kuuawa mwaka wa 2025 wakati wakisubiri kupokea msaada wa chakula kutoka kwa kile kinachoitwa Taasisi ya Misaada ya Kibinadamu wa Gaza, inaoendeshwa kwa pamoja na Marekani na Israel.

Ripoti ya CNN, ikitegemea uchambuzi wa video, picha za setilaiti na simulizi kutoka kwa mashahidi na wanajeshi wa zamani wa Israel, inaangazia kwamba Israel ilihusika katika uvunjaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu huko Gaza.

Uchunguzi huo unaonyesha hali ngumu na mashaka yaliyowapata Wapalestina waliotoweka walipokuwa wakijaribu kufika kwenye misafara ya misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Gaza.

Manusura na familia za waliotoweka zimesimulia matukio ya ukatili yaliyofuatana na milio ya risasi isiyo ya kawaida kutoka kwa wanajeshi wa Israel, huku raia waliokata tamaa wakijitahidi kupata chakula.

Mwanajeshi wa Israel ameiambia CNN kwamba kikosi chake kiliwazika Wapalestina tisa wasio na silaha bila kuashiria makaburi yao au kuorodhesha utambulisho wao kupitia picha.

Mwanajeshi huyo wa Israel ameelezea jinsi harufu ya miili iliyooza ya Wapalestina ilivyofikia kiwango kisichovumulika huku mbwa wakitafuta mabaki ya miili hiyo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Med Human Rights Monitor pia limerekodi vitendo hivyo kupitia programu ya kimfumo, likitumia uchunguzi wa uwanjani kaskazini na kusini mwa Gaza.

Ripoti za shirika hilo zinaonyesha kwamba wanajeshi wa Israel mara nyingi walizika miili ya Wapalestina katika maeneo ya umma, maeneo ya wazi na maeneo ya karibu na vituo muhimu kama vile vituo vya usambazaji wa misaada, hospitali, na shule.

Tangu Oktoba 2023, jeshi la Israel limewaua Wapalestina wasiopungua 70,117, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine 170,999.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *