Rais wa Marekani Donald Trump amewasifu marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda kwa kile alichokiita “ujasiri” wao wa kusaini makubaliano mapya yanayolenga kukomesha mzozo wa muda mrefu mashariki mwa Kongo DR na kufungua njia ya kuchotwa rasilimali muhimu za madini katika eneo hilo na Marekani na makampuni ya Kimarekani.

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika mjini Washington, ilimpa Trump fursa nyingine ya kujitangaza kama msuluhishi na mleta makubaliano wa kimataifa. Rais huyo wa Marekani, ambaye ameelezea mara kwa mara kiu yake ya kutaka atunukiwe Tuzo ya Amani ya Nobel, aliuita mkataba huo kama ushindi wa kidiplomasia.

“Ni siku nzuri kwa Afrika, siku nzuri kwa dunia,” alitangaza Trump na kuongezea kwa kusema, “leo, tunafanikiwa ambapo wengine wengi wameshindwa.”

Marais Félix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda walisafiri hadi mji mkuu huo wa Marekani kwa ajili ya utiaji saini huo, ambapo waliungana na viongozi kutoka mataifa mengine ya Afrika.

Hafla hiyo imefanyika katika wiki hii ambapo Trump ametoa hadharani matamshi ya dharau na matusi dhidi ya nchi ya Kiafrika ya Somalia, akisema hataki wahamiaji kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki waingie Marekani.

Ikulu ya White House imeelezea makubaliano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda kuwa ni “ya kihistoria,” yakitokana na hatua za miezi kadhaa ya upatanishi uliohusisha Marekani, Umoja wa Afrika na Qatar.

Hayo yanajiri huku mapigano yakiendelea kuripotiwa wiki hii huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Bado tuko vitani,” amesema Amani Chibalonza Edith, mkazi wa Goma mwenye umri wa miaka 32 akiongezea kwa kusema: “hakuwezi kuwepo na amani maadamu kungali kuna mapigano katika safu za mbele za vita”.

Marais wenyewe wa DRC na Rwanda wameyakaribisha kwa tahadhari makubaliano hayo ya Washington…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *