Spika wa Bunge la Iran, Mohammad-Baqer Qalibaf amesema ingawa Iran iko wazi kwa diplomasia, lakini haitalegeza kamba katika suala la usalama wa taifa na nguvu zake za ulinzi.

Qalibaf alitoa matamshi hayo jana katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Siasa ya Bunge la Asia (APA) katika mji mtakatifu wa Mash’had.

Spika wa Bunge la Iran alisisitiza kwamba diplomasia ya kweli inaweza kuwa na maana tu inapojengwa katika heshima ya pande zote na maslahi ya pamoja, si kwa kulazimishwa au vitisho.

“Ninasema wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaweka usalama wake wa taifa, uwezo wake wa kujilinda na haki yake halali ya kupiga hatua za maendeleo kwenye meza ya mazungumzo,” amesema Spika Qalibaf.

Spika wa Bunge la Iran pia ameeleza kuwa taifa la Iran limekuwa likikabiliwa na “moja ya kampeni kali na zilizopangwa kimfumo za uadui” katika historia ya sasa, ikiwa ni pamoja na kupitia vikwazo visivyo vya kibinadamu, njama za kuzuia maendeleo ya kisayansi na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani, na, hatimaye, mashambulizi ya kiwoga ya Israel na Marekani mapema mwaka huu.

Qalibaf amesema, mashambulio hayo haramu yalitokea katikati ya mazungumzo ya kidiplomasia, lakini baadhi ya serikali za nchi za Ulaya zilichagua kusimama pamoja na wachokozi badala ya kulaani uchokozi huo.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amesema: “Mienendo ya serikali za Magharibi imeonyesha wazi kwamba, kwao, mazungumzo si chombo halisi cha utatuzi wa migogoro, bali ni chombo cha udanganyifu, ucheleweshaji na kulazimisha (matakwa yao).”

Vilevile amelaani “mauaji ya kimbari ya kimfumo” yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza, ambayo yameua zaidi ya Wapalestina 70,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *