Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametoa indhari kuhusu hatari ya kuzuka wimbi jipya la ukatili katika eneo la Kordofan, Sudan, baada ya kushadidi mapigano kati ya Jeshi la Sudan (SAF), Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) na Kundi la Harakati ya Kaskazini ya Ukombozi wa Wananchi wa Sudan, (SPLM-N).

Türk, ametoa indhari hiyo kufuatia kuripotiwa vifo vya zaidi ya watu 269 vilivyosababishwa na mashambulizi tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa raia wengi wanashikiliwa kwa tuhuma za “kushirikiana” na upande pinzani, huku kukiongezeka hotuba za chuki pia zinazochochea machafuko zaidi.

Taarifa kutoka Geneva, Uswisi imeeleza kuwa tangu tarehe 25 Oktoba na baada ya RSF kuuteka mji wa Bara, Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN imeorodhesha vifo vya raia wasiopungua 269 kutokana na mashambulizi ya angani, mabomu ya ardhini na mauaji ya kiholela. Idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na kukatika mawasiliano na intaneti, jambo linalozuia taarifa sahihi kupatikana.

Ripoti zinaonesha pia kuwepo kwa ulipizaji kisasi, ukamatwaji watu kiholela, utekaji nyara, ukatili wa kingono na ulazimishaji watu ikiwemo watoto kujiunga na makundi ya kivita.

Kwa majuma ya hivi karibuni, mashambulizi kadhaa yameripotiwa, ikiwemo shambulio la ndege zisizo na rubani la RSF la tarehe 3 mwezi Novemba katika mji wa El Obeid lililoua watu wapatao 45, wengi wao wakiwa wanawake, na shambulio la anga la SAF tarehe 29 Novemba katika eneo la Kauda lililosababisha vifo vya karibu watu 48.

Mapigano makali yanaendelea katika majimbo yote matatu ya Kordofan, na kusababisha vifo na majeruhi zaidi.

Zaidi ya watu 45,000 wamelazimika kukimbia makazi yao mwezi uliopita, wakitafuta usalama ndani au nje ya Kordofan.

Kamishna Türk amezitaka pande zote katika mzozo nchini Sudan kusitisha mapigano mara moja, kuruhusu misaada ya dharura, kulinda wahudumu wa kibinadamu na kurejesha mawasiliano ili taarifa muhimu ziweze kuwafikia raia.

Aidha, ametoa wito kwa nchi zenye ushawishi kuingilia kati, kusitisha mtiririko wa silaha na kusaidia kumaliza mapigano.

“Hatuwezi kuruhusu Kordofan kuwa mwendelezo wa maafa tuliyoyaona El Fasher. Vita lazima vikome sasa,” amesisitiza Mkuu huyo wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *