
Mitaa ya mji mkuu wa Iraq, Baghdad usiku wa kuamkia leo ilishuhudia misafara mirefu ya magari, yaliyokuwa yakipeperusha bendera za harakati za Muqawama wa Kiislamu za Hizbullah ya Lebanon na Ansarullah ya Yemen, na kutangaza mshikamano wa umma na harakati hizo za Muqawama dhidi ya vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Harakati hiyo ya kialama imeonyeshwa kama ishara ya uungaji mkono wa waanchi wa Iraq kwa Mhimili wa Muqawama kufuatia mivutano iliyozuka hivi karibuni na kufuatia kuchapishwa orodha ya mali zilizozuiliwa na serikali ya nchi hiyo za harakati za Hizbullah na Ansarullah.
Tukio hili limejiri baada ya mamlaka za fedha za Iraq kuchapisha kimakosa katika magazeti rasmi ya nchi hiyo orodha inayoonyesha kuwa harakati za Hizbullah ya Lebanon na Ansarullah ya Yemen zimejumuishwa katika listi ya makundi ya kigaidi ambayo mali zao zitazuiliwa na serikali ya Baghdad.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, maandamano hayo ya misafara ya magari ya wananchi wa Iraq kama mojawapo ya mijibizo ya kuonyesha uungaji mkono wa wananchi hao kwa mhimili wa Muqawama na kusisitizia kuwepo kwa msimamo mmoja wa kukabiliana na njama chafu za utawala wa Kizayuni katika eneo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Iraq Muhammad Shia al-Sudani ameamurukufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu jambo hilo na kutambuliwa maafisa waliohusika na kosa hilo na kuchukuliwa hatua.
Al-Sudani amesisitiza kwamba uamuzi wa awali wa kuchapisha orodha hiyo ulijumuisha watu binafsi na makundi yanayohusiana na DAESH na Al-Qaeda pekee, na kwamba kujumuisha majina ya harakati za Hizbullah na Ansarullah kwenye orodha hiyo ilikuwa kosa ambalo halikukusudiwa.
Kwa upande mwingine, Benki Kuu ya Iraq nayo pia imetoa amri ya kuondolewa majina ya harakati hizo za Muqawama kwenye orodha ya mali za kigaidi, ikisisitiza kwamba kuingizwa majina hayo kulifanywa kimakosa…/