Utafiti mpya unaonyesha kwamba wasichana na wanawake nchini Uingereza bado wanahisi hawako salama katika maeneo ya umma.

Elish Angiolini, mkuu wa Timu ya Uchunguzi wa Mauaji ya Sarah na wakili maarufu wa Scotland, ameonya kwamba wawindaji wa wanawake nchini Uingereza wanaendelea kuzurura kwa uhuru na kwamba wasichana na wanawake nchini humo wanaishi kwa hofu ya mashambulizi katika maeneo ya umma, miaka minne baada ya mauaji ya Sarah.

Sarah Everard alibakwa na kuuawa na afisa wa polisi wa London, Wayne Couzens, ​​​​mnamo Machi 2021. Mauaji hayo ya kutisha yaliwakasirisha sana watu wa Uingereza na kusababisha maandamano makubwa. Uchunguzi wa mauaji ya Sarah Everard nchini Uingereza unaonyesha kwamba miaka minne baada ya tukio hilo, wanawake na wasichana bado wanahisi hawana usalama katika mitaa ya miji ya nchi hiyo.

Ripoti zinasema, wanawake wengi wamekuwa wakishambuliwa na wanaume tangu kesi hiyo ilipoanza mwaka wa 2021, na kwamba kuna “mapungufu ya msingi” katika kurekodi taarifa za awali kuhusu mashambulizi na kufeli vyombo vya dola kuzuia mashambulizi dhidi ya wasichana na wanawake.

Ripoti ya Angiolini imesema kwamba hakuna takwimu maalumu kuhusu uhalifu unaosababishwa na ukatili wa kingono dhidi ya wanawake katika maeneo ya umma, jambo ambalo ni pengo linalotia wasiwasi katika utungaji sera na mipango ya usalama wa wanawake.

Ripoti ya mkuu wa Timu ya Uchunguzi wa Mauaji wa Sarah inasema kwamba sehemu kubwa ya wanawake nchini Uingereza, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, wafanyakazi, polisi wanawake, n.k., wako katika hali ya tahadhari ya kudumu kutokana na ongezeko la ukosefu wa usalama katika maeneo ya umma.

Asilimia 71 ya wanawake Uingereza wamepitia ukatili wa kingono

Katika sehemu moja ya ripoti yake, Angiolini amenukuu utafiti wa Umoja wa Mataifa uliohusisha zaidi ya wanawake elfu moja nchini Uingereza, akisema kwamba karibu asilimia 71 ya wanawake hao walisema wamepitia aina fulani ya unyanyasaji au ukatili wa kingono katika maeneo ya umma, kwa uchache mara moja katika maisha yao.

Wakati huo huo, wabunge kadhaa wanawake katika Bunge la Uingereza wamesema kwamba huvaa viatu vya michezo wanapotoka nyumbani ili waweze kukimbia kwa urahisi wanapokabiliwa na mashambulizi ya kikatili kutoka kwa wanaume, na huwa wanazungumza na rafiki zao kwa simu wanapokuwa peke yao nje ya nyumba ili wajisikie salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *