
Yasser Abu Shabab, mshirika wa kijeshi wa utawala wa kizayuni wa Israel mwenye uhusiano pia na kundi la kigaidi la DAESH (ISIS), maarufu kwa kuongoza uporaji wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza na kwa kuwalenga raia wa Palestina, ameripotiwa kuuawa katika eneo hilo.
Vyombo kadhaa vya habari vya Israel vimeripoti kuuawa kwa Abu Shabab hapo jana Alkhamisi, lakini bila ya kuweka wazi nani aliyehusika na mauaji yake au mazingira yaliyotokea mauaji hayo.
Tukio hilo linasemekana lilitokea huko Rafah kusini mwa Ghaza, eneo ambalo kwa sasa liko chini ya udhibiti kamili wa jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel.
Chaneli ya Israel 12 awali iliripoti kwamba Abu Shabab alikuwa amepelekwa Hospitali ya Soroka baada ya kujeruhiwa, ambapo baadaye alitangazwa kuwa amekufa. Hata hivyo, hospitali hiyo ilikana kumpokea gaidi huyo.
Mwandishi wa habari wa Channel 12 Amit Segal ameelezea mauaji yaliyoripotiwa ya Abu Shabab kama “mabadiliko mabaya kwa Israel,” akitilia mkazo jukumu alilokuwa akitekeleza la kuwa mshirika wa utawala huo kutoka miongoni mwa Wapalestina.
Abu Shabab aliibuka wakati wa vita vya mauaji ya kimbari vya miaka miwili kama mkuu wa kile kilichoitwa Vikosi vya Wananchi, akipora misaada na kuwaua au kuwateka nyara raia wa Palestina na wapiganaji wa Hamas pamoja na kushirikiana na vikosi vya jeshi la kizayuni.
Imeripotiwa kwamba alikuwa akizatitiwa kwa silaha na kupewa uhuru wa kuendesha harakati zake chini ya ulinzi wa kijeshi wa Israel.
Abu Shabab aliandamwa na lawama nyingi kutoka makundi ya Wapalestina, ambao walimuona yeye na kundi lake kama wasaliti na kulihusisha na Israel na Daesh.
Alikuwa amefungwa jela na serikali ya Palestina huko Ghaza kwa miaka kadhaa kwa mashtaka yanayohusiana na madawa ya kulevya kabla ya kutoroka gerezani mwanzoni mwa vita vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni dhidi ya eneo hilo la Palestina.
Abu Shabab alichukiza hata mbele ya watu wa kabila lake mwenyewe, ambao wameeleza katika taarifa kwamba mauaji yake ni “mwisho wa taswira chafu ambayo haiwakilishi historia ya kabila hilo”…/