London, England. Kuanzia Jumapili wiki hii, nyasi za viwanja tofauti Morocco zitaanza kuwaka moto kwa uwepo wa mechi za Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, kila timu ya taifa inayoshiriki inatakiwa kuwasilisha orodha ya wachezaji wasiozidi 28 ambao watatumika katika fainali hizo.

Wakati timu nyingi za taifa zinazoshiriki AFCON 2025 zikiwa zimeshaanza kupata wachezaji wao mbalimbali ambao zimewaita kwa ajili ya mashindano hayo, uteuzi wa nyota hao unaziacha baadhi ya klabu katika mtego.

Klabu hizo zitalazimika kuendelea na michezo ya ligi na mashindano mengine tofauti katika nchi zao pasipo uwepo wa wachezaji hao ambao watakuwepo Morocco wakizitumikia timu zao za taifa.

Ligi Kuu England ni miongoni mwa Ligi ambazo zimetoa idadi kubwa ya wachezaji ambao watashiriki AFCON 2025 huko Morocco na hapana shaka hilo limechangiwa na ubora wa ligi hiyo.

Wakati Ligi hiyo ikiendelea, baadhi ya klabu zake zitawakosa jumla ya nyota 25 ambao watakuwepo Morocco, jambo ambalo linaweza kuwa na athari kwa klabu hizo katika mechi ambazo zitacheza kipindi cha mashindano hayo.

Sunderland ndio timu ambayo inaachiwa maumivu zaidi na AFCON kwani wachezaji wake watano wameitwa kucheza fainali hizo ambao ni Chemsdine Talbi (Morocco), Reinildo (Mozambique), Bertrand Traoré (Burkina Faso), Arthur Masuaku (DR Congo) na Noah Sadiki (DR Congo).

Manchester United, Fulham na Burnley zifuatia kwa kutoa wachezaji wengi ambapo kila moja imetoa wachezaji watatu.

Nyota wa Manchester United ambao watakuwemo AFCON ni Bryan Mbeumo (Cameroon), Amad Diallo (Ivory Coast) na Noussair Mazraoui (Morocco), Fulham ikiwa na Alex Iwobi, Calvin Bassey na Samuel Chukwueze, wote wakiitumikia Nigeria.

Wachezaji watatu wa Burnley ni Axel Tuanzebe (DR Congo), Lyle Foster (Afrika Kusini), na Hannibal Mejbri (Tunisia).

Nottingham Forest, Brentford, Wolves, Crystal Palace na Man City, kila moja ina wachezaji wawili katika fainali hizo.

Nyota wa Nottingham Forest ni Ibrahim Sangaré na Willy Boly wa Ivory Coast, Brentford imewatoa Dango Ouattara (Burkina Faso) na Frank Onyeka (Nigeria), Wolves itakuwa na Tawanda Chirewa (Zimbabwe) na Emmanuel Agbadou (Ivory Coast), Crystal Palace itawakilishwa na Ismaïla Sarr (Senegal) na Cheick Doucouré (Mali) huku Manchester City ikiwa na Omar Marmoush wa Misri na Rayan Ait Nouri wa Algeria.

Timu zilizotoa mchezaji mmojammoja ni West Ham iliyo na Aaron Wan-Bissaka wa DR Congo, Brighton ina Carlos Baleba wa Cameroon na Liverpool imemtoa Mohamed Salah kwenda Misri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *