Manchester, England. Meneja wa Manchester United, Ruben Amorim, amekiri wachezaji wake waliondoka uwanjani wakiwa na hisia tofauti baada ya kulazimishwa sare ya mabao 4-4 dhidi ya Bournemouth, huku akibainisha maeneo mawili makubwa yanayohitaji maboresho ya haraka.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Old Trafford, Man United ilicheza mpira wa kuvutia ikiongoza mara tatu, lakini ilishindwa kumaliza mchezo na hatimaye ikaruhusu Bournemouth kurejesha mabao.

“Ukifuatilia klabu hii kama ambavyo nimefuatilia Ligi Kuu kwa muda mrefu, una wajibu siyo tu wa kushinda bali pia kucheza kwa namna inayowapa furaha mashabiki.

“Mashabiki wanataka ushindi, lakini pia wanataka kuhamasishwa. Leo (jana) tulihamasisha, lakini pia kuna maumivu ya kutoshinda,” amesema Amorim.

Amorim pia amesema pamoja na mazuri mengi waliyoona, bado kuna kazi kubwa mbele yao.

“Tunapaswa kuelewa vizuri mwelekeo wa mchezo na kuwa wakali zaidi mbele ya lango. Tulitengeneza nafasi nyingi za kushinda, kwa hiyo tulipaswa kupata pointi tatu,” amesisitiza Amorim.

Kocha huyo aliongeza kuwa pamoja na United kucheza soka linalofurahisha zaidi msimu huu, bado tatizo kubwa lipo katika ulinzi.

“Tunakosa ubora wa kutosha tunapolinda lango letu. Hilo ni jambo lazima tulishughulikie haraka,” amesema.

Hali inazidi kuwa ngumu kwa Amorim kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa Jumapili, ambapo atawakosa wachezaji sita.

Mabeki Harry Maguire na Matthijs de Ligt bado ni majeruhi, Casemiro atasimamishwa baada ya kupata kadi tatu za njano, huku Noussair Mazraoui, Amad Diallo na Bryan Mbeumo wakielekea kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

“Huo ndiyo uzuri na changamoto ya kazi ya ukocha. Tutatafuta suluhisho kwa wachezaji tulionao. Tuko tayari kukabiliana na hali,” amesema Amorim.

Mfungaji wa bao la kwanza wa United, Amad Diallo, ameeleza hali ilivyokuwa ndani ya chumba cha kubadilishia nguo.

“Tumesikitishwa sana kama timu. Tunajua tunapaswa kufanya vizuri zaidi. Kama tungeshinda leo, tungekuwa kwenye nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo wa ligi. Kila mmoja amevunjika moyo,” amesema Diallo.

Kwa upande wa Bournemouth, kocha Andoni Iraola alifurahishwa na mapambano ya kikosi chake, lakini alionesha wasiwasi juu ya kiungo Tyler Adams aliyelazimika kutoka mapema baada ya kuumia goti la kushoto akizuia shuti la Matheus Cunha.

“Hizi ndizo habari mbaya zaidi kutoka kwenye mchezo. Alipinda goti, bado hatujajua kama ni jeraha dogo au kubwa. Kumpoteza mchezaji kama Tyler ni pigo kubwa sana kwetu,” amesema Iraola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *