Dar es Salaam. Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden umetoa wito kwa Watanzania wenye sifa kuchangamkia fursa za masomo ya uzamili kwa mwaka wa masomo 2026/27 nchini humo, ili kuongeza idadi ya wanaonufaika na udhamini wa Taasisi ya Sweden (Swedish Institute – SI).

Wito huo umetolewa na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, akieleza kuwa kwa mwaka wa masomo wa 2025/26, Tanzania ilinufaika kwa kupata nafasi 11 pekee za ufadhili, idadi inayotajwa kuwa ndogo ikilinganishwa na mataifa mengine yanayopata hadi nafasi 40.

Amesema taarifa hiyo ilibainika baada ya kikao kilichofanyika Oktoba 29, 2025, kati yake na uongozi wa Taasisi ya Sweden, akiwamo Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Kimataifa ya SI, Kurt Bratteby, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Programu ya Ufadhili wa Masomo na Uongozi, Adiam Tedros.

Kwa mujibu wa Balozi Matinyi, uongozi wa SI ulimueleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotuma maombi machache ya wanafunzi kila mwaka, hali inayochangia kupata nafasi chache za ufadhili ikilinganishwa na mataifa mengine.

“Kutokana na hali hiyo, niliuomba uongozi wa SI utoe kipaumbele kwa Watanzania wenye sifa watakaoomba kwa mwaka huu, huku Ubalozi ukiahidi kuhakikisha taarifa za fursa hizi zinawafikia Watanzania wengi zaidi ili kuongeza idadi ya waombaji,” amesema.

Ameeleza kuwa kwa mwaka huu wa masomo, fursa za ufadhili zimejikita katika maeneo ya taaluma ya utawala, afya ya umma, ujasiriamali na ubunifu, pamoja na sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

Balozi Matinyi amefafanua kuwa waombaji wanapaswa kuanza kwa kuomba udahili katika vyuo vikuu vya Sweden kupitia tovuti rasmi ya University Admissions ifikapo Januari 15, 2026.

“Baada ya kupata udahili, ndipo mwombaji ataendelea kuomba ufadhili wa masomo kupitia tovuti ya Taasisi ya Sweden hadi Februari 26, 2026,” amesema.

Hata hivyo, amewashauri Watanzania wanaohitaji maelezo ya ziada kuhusu fursa hizo kuwasiliana moja kwa moja na Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden kupitia anuani yao ya barua pepe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *