
Nyota wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher amemtaja mshambuliaji Phil Foden wa Manchester City kama mchezaji tishio zaidi kwa Arsenal katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu huu.
Jana Jumapili, Desemba 14, 2025, foden alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-0 ambao Man City iliupata ugenini dhidi ya Crystal Palace huku mengine mawili yalipachikwa na Erling Haaland.
Lilikuwa ni bao la sita kwa Foden katika mechi nne zilizopita za EPL na Carragher anaamini kwamba makali ya mchezaji huyo yanaweza kuiweka Arsenal katika wakati mgumu zaidi.
“Alikuwa ni Mchezaji Bora wa msimu mwaka mmoja uliopita lakini hakuwa yeye kwa sababu yoyote msimu uliopita. Lakini sasa anaonekana kuwa kwenye ubora wake.
“Amerudi katika ubora na ni mmoja kati ya wachezaji bora wa EPL na ninaendelea kusema kama sio Haaland (Erling), ni yeye anayetakiwa kuhofiwa zaidi na Arsenal.
“Haaland anategemewa. Anafanya hivyo kila mwaka akifunga mabao 30 hadi 40. Na anafanya hivyo msimu huu lakini Phil Foden kurudi katika sherehe kiuhalisia ni hatari,” amesema Carragher.
Kwa upande mwingine, Carragher amemsifu meneja wa Aston Villa, Unai Emery akidai kwa sasa anazidiwa na Pep Guardiola tu katika EPL.
“Nimesema leo (jana) kuwa nadhani ni Pep Guardiola pekee kwa sasa ambaye ni meneja bora zaidi kumzidi Unai Emery.
“Ukiangalia wasifu wake na nini alichokifanya katika kazi yake ya umeneja. Kuna baadhi ya mameneja bora lakini kama nilivyosema, ana wsifu mkubwa. Amefanya kanzi nzuri,” amesema Carragher.