Dar es Salaam. Kama kuna kiungo ambaye bado mpira wa miguu unamuhitaji ni Himid Mao Mkami lakini umri ndiyo changamoto ambayo inafanya kiungo huyo wa ukabaji kuhesabiwa siku za kuachana na soka.

Nyota huyo alianzia maisha yake ya soka ndani ya Klabu ya Azam FC mwaka 2009 baada ya kupandishwa katika kikosi cha wakubwa akitokea katika kikosi cha vijana ‘Azam ambacho alikifanyia makubwa ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Vijana chini ya umri wa miaka 2o ‘Uhai Cup’ mara mbili mfululizo.

Himid mwenye umri wa miaka 33, alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Azam waliotwaa taji la kwanza la Ligi Kuu msimu wa 2013/2014 na aliondoka kwa matajiri hao wa Chamazi mwaka 2018 ambapo alielekea Misri kujiunga na Klabu ya Petrojet.

Aliitumikia kwa msimu mmoja kisha akajiunga na Enppi SC ya hukohuko ambayo nayo alihudumu kwa mwaka mmoja. Akiwa Misri alitumikia klabu tano tofauti.

Kiungo huyo alirejea Azam FC msimu huu kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika katika Klabu ya Talaea El Gaish ambayo ndiyo ilikuwa timu yake ya mwisho kuichezea huko Misri. Hata hivyo, mkongwe huyo bado anaonekana kuwa moto wa kuotea mbali kwani tangu ajiunge na kikosi cha Azam FC amekuwa mchezaji wa kutegemewa na kocha, Florent Ibengé.

Hadi sasa Himid ameisaidia Azam FC kutinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika akiingia kwenye historia ya kuwa miongoni mwa wachezaji waliyoipeleka timu hiyo katika hatua ya makundi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004.

Ikumbukwe kuwa kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo raia wa Brazil, ndiye aliyemuibua Himid katika Kituo cha Kukuza Vipaji cha TSA na kumjumuisha mara kadhaa katika kikosi cha wakubwa kupata uzoefu.

Alitamani Ulaya

Kiungo huyo ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Mao Mkami, alikuwa na ndoto ya kucheza soka la kulipwa Barani Ulaya, hata hivyo, alipoenda kujiunga na Petrojet ya Misri nyota huyo alisema ilikuwa njia ya kuingia Ulaya licha ya kutopata nafasi hiyo;

“Lengo lilikuwa kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini mambo yamekwenda tofauti kwa hiyo imebidi niwe na njia mbadala ambayo ni kupitia huku Misri ambako wachezaji wengi wanaofanya vizuri wanakwenda kwa wepesi.

“Ilibidi nije huku kumalizana nao kwa sababu walionyesha nia ya kunihitaji muda mrefu nilivyofika tulikubaliana baadhi ya mambo na kusaini,” alisema Himid.

Mchezaji huyo alidokeza changamoto nyingine ambazo ni tofauti ya vyakula kati ya wenyeji wageni.

Joto pia ni miongoni mwa changamoto ambazo Himid amekutana nazo Misri, lakini amekuwa akipambana nalo kwa kuwa ni sehemu ya maisha.

 Hata hivyo Himid anasema kwamba msaada mkubwa kutoka kwa wachezaji wenzake mara baada ya yeye kufika Misri, ulichangia kwa kiasi kikubwa azoee kwa haraka maisha ya nchi hiyo.

Azam iko vizuri

Akizungumzia kuhusu kiwango cha Azam FC katika kushindania mataji ya ndani na Kimataifa, Himid alisema wana nafasi nzuri kwenye Ligi Kuu kutokana na ubora wanaouonyesha pia wanatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa timu pinzani.

“Haitakuwa rahisi lakini najivunia kuwa sehemu ya kikosi ambacho kimeandika historia kimataifa na ubora mkubwa unaoonyeshwa na wachezaji ni ukomavu walionao baada ya kukosa kwa misimu mingi, naona kikosi kikiimarika.

“Wachezaji waliopo wana ukomavu wa hali ya juu hapa tulipofika itabaki historia na bado tunahitaji kuwa na mwendelezo bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuona Azam FC siku moja inaleta taji la Afrika hili linawezekana tumesahau yaliyopita tumerudi kwenye ushindani mpya.

“Furaha ya kufuzu hatua ya makundi tumeshaisahau tunarudi Ligi Kuu kusaka nafasi ya uwakilishi kimataifa msimu ujao ili kuendelea kujijengea uhakika wa kupata uwakilishi na hatimaye kutwaa mataji ya Afrika.

“Tunafahamu ugumu uliopo kwenye ligi kutokana na sajili bora zilizofanywa na wapinzani, lakini hilo halituondoi kwenye malengo, tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha mambo yanaenda kama tulivyopanga,” alisema Himid.

Kundi Kombe la Shirikisho

Akizungumzia droo ya Kombe la Shirikisho Afrika alisema wamepangwa kundi bora na matarajio ni kuona wanafanya vizuri kwa kupata nafasi ya kutinga hatua inayofuata.

“Timu zote ni bora na shindani na ndiyo maana zimefika hatua hiyo. Hakuna mteremko mipango imara na ubora wetu ndiyo utaamua ni timu gani itaenda hatua inayofuata. Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kuipambania nembo ya klabu.

“Ukizingatia tupo na benchi bora la ufundi ambalo lina uzoefu mzuri na michuano ya mikataifa imani yetu ni kubwa tutakuwa bora na kutinga hatua inayofuata bila kuangalia tunashindana na nani sisi tunaamini katika kujiandaa vyema na kutumia kila nafasi tutakayotengeneza ili kufikia malengo,” alisema kiungo huyo.

Ikumbukwe kwamba kwa sasa, Azam FC inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi B la mashindano hayo ikiwa haina pointi.

Himid ni wa mtoto wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto watano akiwa na ndugu zake Femina, Rozmana, Feisal na Rahim.

Elimu yake ya msingi alipata katika Shule ya Msingi Kiwandani, Turiani, Morogoro darasa la kwanza na la pili na kuhamia Karume ya Dar es Salaam aliposoma hadi darasa la sita.

Mchezaji huyo alihama na kumalizia elimu ya msingi katika Shule ya Msingi ya Dk. Omary Ali Juma iliyopo Magomeni, Dar es Salaam kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tabata ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 2011.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *