Dar es Salaam. Bala Hatun anayefananishwa na mfano wa mwanamke shupavu katika historia ya dola ya Ottoman, amekuwa mmoja wa wahusika muhimu zaidi katika mfululizo wa tamthilia ya The Ottoman.

Kuigiza kwa uhalisia kumemfanya Bala ajizolee umaarufu mkubwa Uturuki na nchi zingine zinazofuatilia tamthilia hiyo.

Bala ambaye kabla ya kuigiza kwenye tamthilia hiyo hakuwa ametambulika sana kimataifa, ameibuka kama mmoja wa waigizaji mahiri wa kizazi kipya.

Uhusika wa Bala akicheza kwa hisia za upole, hekima, ujasiri na uchungu wa maisha ya vita akionyesha huzuni usoni, uthabiti kwa mwili na upendo wa kweli.

Kwenye moja ya mahojiano alisema baada ya kuchaguliwa kuigiza kwenye tamthilia hiyo alilazimika kuanza kuifuatilia histori ya mke wa himaya ya Ottoman, Osman Bey kwa undani zaidi ili angalau aweze kucheza kama historia ya taifa hilo.

“Nilipochaguliwa nikajisemea moyoni naweza kuifanya hii kweli, lakini nikasema nitaweza kwa kuwa ilikuwa scene yangu ya kwanza kubwa na nacheza kama muhusika mkuu nilijiuliza watu wanataka kumuona Bala Hatun yule wa kwenye vitabu vya historia ya Uturuki,” alisema Bala Hatun

“Kwa hiyo nikamsoma zaidi ili nisipate ugumu zaidi nikauvaa uhusika wa mtoto wa Sheikh Edebali nafikiri kuna vitu tunafanana kati yangu mimi na Bala Hatun hasa kwenye mambo ya mamlaka ila kwenye uvumilivu kidogo sina ustahmilivu.”

Ubora wake unadhihirika kwenye kila tukio kuanzia namna anavyoshika upanga, anavyohutubia wanawake wa Kayi, hadi alivyo tayari kusimama mstari wa mbele kwa ajili ya haki ya watu wake.

“Kabla sikuwahi kushika panga kwa ukubwa kiasi kile lakini farasi nimewahi kupanda nilipotoka na familia yangu, hivyo tulichukua kama miezi mitatu ya mafunzo ya kushika panga, kurusha mishale na hata kuzoea kuvaa mavazi ya mke wa Bey.”

Bala Hatun si tu mke wa Osman, lakini ni mshauri wa kisiasa, mwalimu wa kiroho na nguzo ya familia. Anatumiwa kama daraja kati ya masuala ya dunia ya Kayi na mafundisho ya dini na maadili yaliyoasisi dola mpya.

Migongano mikubwa ya kisiasa na vita vya kihisia vinavyomkumba ikiwemo ushindani wa kindoa, maumivu ya kupoteza wapendwa, na kupambana kuendeleza falsafa ya baba yake Sheikh Edebali vimeifanya nafsi ya Bala kuwa yenye tabaka nyingi kuliko wahusika wengi wa kike katika kazi za Kituruki.

Kolabo yake na Osman Bey

Bala ni mwanamke anayepambana bega kwa bega na wanaume katika maeneo ya uongozi, vita, na majadiliano ya hatima ya ukoo.

Katika mazingira ya karne ya 13, ambako wanawake walikuwa wakifichwa nyuma ya familia, Bala anaonekana kama kielelezo cha kubadilisha historia na kumsaidia mumewe.

Mwanadada huyo amekuwa na kolabo nzuri na Osman Bey (Burak Özçivit) ambaye kwenye tamthilia hiyo ni mume wake aliyekuwa nyuma ya mafanikio ya kiongozi huyo wa Wakayi.

Uhusiano wao umekuwa moja ya sababu ya mafanikio ya tamthilia hiyo. Wawili hawa wanaleta mchanganyiko wa mapenzi tulivu, maumivu ya kupoteza watoto na changamoto za kisiasa.

Kolabo yao imewafanya baadhi ya mashabiki wahisi ni kweli upendo wa kweli wa wawili hao ni halisi kumbe kila mmoja ana maisha yake mengine nje ya tamthilia ambapo Osman ana mke na Bala hajaripotiwa kuwa na uhusiano.

Bala Hatun ni nani?

Jina lake kamili ni Ozge Torer alizaliwa Agosti 16,1999 jijini Izmir nchini Uturuki ni miongoni mwa watoto watatu kwenye familia yao akiwa na wadogo zake Berkay na Onder.

Alisoma katika Chuo Kikuu cha Mugla Sitki Kocman, ambapo alihitimu kutoka Fakulteti ya Sanaa za Utendaji (Fine Arts), akijikita kwenye uigizaji wa tamthilia.

Wakati wa chuo, aliibuka katika tamthilia za shule na hata kupata tuzo ya uigizaji bora wa jukwaa, ikionesha uwezo wake wa asili katika sanaa ya uigizaji.

Kazi
Ukiachana na kazi za uigizaji alizowahi kuzifanya chuoni The Ottoman (2019) ndio kazi pekee alipopewa nafasi ya Bala Hatun katika mfululizo huo hadi sasa inapoendelea.

Nje ya Ottoman hakuna kazi nyingine mpya aliyocheza mwanadada huyo hivyo ndio kazi pekee iliyomfanya atambulike duniani.

Kazi moja tu ya The Ottoman imempa Bala Hatun tuzo nne za muigizaji bora Crystal Globe Awards mwaka 2020 kama Best Actress of the Year akishinda kupitia uhusika wa Bala Hatun.

Tuzo nyingine ni Eurasian Consumer Protection Association Award 2021 kama Best Actress of the Year (Bala Hatun) mwaka huohuo akachukua tena tuzo ya Crystal Globe Awards 2021, Best Actress of the Year (Bala Hatun) na Tuzo ya Chuo Kikuu (University Theater Award).

Maisha binafsi 

Bala Hatun anaishi maisha ya faragha na taarifa zinaeleza bado hajaolewa na hana watoto. Hali ya uhusiano wake haijawekwa hadharani, na anaweka maisha yake binafsi mbali na vyombo vya habari.

Ana uhusiano wa karibu na familia yake, hasa ndugu zake Berkay na Onder, ambao mara kwa mara huonekana akiwataja kwa heshima katika mahojiano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *