London, England. Nahodha wa zamani wa Chelsea, John Terry, amefunguka na kukiri kuwa aliwahi kuwaza kujiua baada ya kukosa penalti katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008 dhidi ya Manchester United.

Terry aliteleza na kupiga mpira kwenye mwamba wa lango katika penalti ambayo ingeipa Chelsea ubingwa kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Luzhniki, Moscow.

Manchester United baadaye waliibuka washindi wa mikwaju ya penalti, tukio ambalo limeendelea kubaki kumbukumbu chungu katika maisha ya beki huyo wa zamani.

Akizungumzia tukio hilo Terry (45) amesema baada ya mchezo huo mawazo mazito yalimpitia kiasi cha kufikiria kujirusha kutoka ghorofa ya 25 ya hoteli waliyokuwa wamefikia Moscow.

“Kwa kweli ningependa wakati ule ningezungumza na mtu. Nakumbuka baada ya mchezo tulirudi hotelini, nilikuwa ghorofa ya 25 nikiangalia dirishani na kujiuliza kwa nini? kwa nini?.

“Sisemi kwamba ningefanya hivyo moja kwa moja, lakini mawazo mengi hupita kichwani wakati kama huo. Bahati nzuri wenzangu walipanda na kunichukua wakanipeleka chini,” amesema Terry.

Terry amesema maumivu hayo yaliendelea hata waliporejea England kwa majukumu ya timu ya taifa, ambapo alilazimika kukaa mezani pamoja na wachezaji wa Manchester United.

“Halafu tukacheza na Marekani, Wembley nikafunga bao, ndipo nikajiuliza kwa nini nisingebadilisha tukio lile la penalti na hili.”

Kwa mujibu wa Terry, hadi leo bado anakumbwa na mawazo ya tukio hilo, hasa baada ya kustaafu soka.

“Wakati unacheza mechi nyingi, unaweka mambo nyuma kidogo. Lakini sasa nimeacha kucheza, sina ile hamasa ya kila wiki, ndipo maumivu yanarudi. Naamka usiku nikikumbuka na nafikiri hayatowahi kuniacha kabisa,” amesema beki huyo wa zamani wa Chelsea.

Baada ya fainali hiyo, Terry aliandika barua ya kuomba radhi kwa mashabiki wa Chelsea na alikiri kulala kwa saa chache tu katika siku zilizofuata, akirudia tukio hilo akilini mara kwa mara.

Miaka minne baadaye, Chelsea ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa kwa penalti dhidi ya Bayern Munich, ambapo Terry alifanikiwa kuinua kombe hilo, ingawa hakushiriki fainali hiyo kutokana na kusimamishwa.

Terry pia alimtaja aliyekuwa kocha msaidizi wa Chelsea, marehemu Ray Wilkins, kama mtu aliyempa msaada mkubwa katika kipindi hicho kigumu.

“Ray alikuwa wa kwanza kunipigia simu kuhakikisha niko sawa. Ni nyakati kama hizi ndipo unatambua rafiki wa kweli ni nani,” amesema.

Wilkins alipofariki mwaka 2018, Terry alimuelezea kama mtu muhimu sana katika maisha yake ya soka na nje ya uwanja.

Akizungumzia namna anavyoishi na maumivu ya tukio hilo, Terry amesema:

“Sijui, unaendelea tu na maisha. Tulikulia kwenye mazingira ya kujikaza na kusonga mbele. Lakini mambo yamebadilika sasa, na hilo ni jambo jema hasa kwa afya ya akili ya wachezaji.”

Kauli hiyo ya Terry imeibua mjadala mpana kuhusu afya ya akili kwa wanamichezo, hasa katika nyakati za presha kubwa na matukio ya kushindwa kufanya vizuri kwenye michezo mikubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *