
Tanzania, Taifa Stars, inakwenda kushiriki AFCON 2026 kwa mara ya nne katika historia yake.
Ilianza 1980 nchini Nigeria. Ikafuatia 2019 kule Misri, halafu 2023 (ilifanyika 2024) kule Ivory Coast na sasa 2026 Morocco.
Bahati mbaya ni kwamba katika mara zote hizi, Stars, haijashinda hata mechi moja
Katika mara hizi zote, ni 2023 pekee ambapo Tanzania ilikaribia kupata ushindi wake wa kwanza, kama sio Zambia kusawazisha dakika ya mwisho ya mchezo.
Sasa inakuja AFCON ya 2026 na Tanzania imepangwa kwenye kundi gumu lenye timu mbili zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa, Tunisia na Nigeria…na jirani mmoja, Uganda.
Kundi hili linarudisha kumbukumbu ya AFCON 2019 kule Misri ambapo pia Tanzania ilipangwa na timu mbili zilizopewa nafasi kubwa ya kuwa mabingwa, Algeria na Senegal, na jirani mmoja, Kenya.
Na kweli, timu zile zikaenda kukutana kwenye fainali…na Algeria wakawa mabingwa.
Kwa kundi hili, na uwezo wetu…badala ya kuwaza hatua za mbele kama 16 bora na kuendelea, sisi tuwaze kupata angalau ushindi wa kwanza kwenye fainali hizi.
Nigeria vs Tanzania – Disemba 23
Hii ni mechi yetu ya kwanza ya mashindano, kama ilivyokuwa 1980 kule Lagos.
Mwaka ule Nigeria wakiwa wenyeji wa mashinda walitufunga 3-1 na wakaenda hadi kutwaa ubingwa…huo ulikuwa ubingwa wao wa kwanza wa AFCON.
Na hadi hapo walikuwa wameshiriki mara tatu tu, 1963, 1976 na 1978.
Hawakuwa wakubwa kimpira barani Afrika kama walivyo sasa…hata matarajio ya watu wao kutwaa ubingwa hayakuwa makubwa kama sasa.
Sasa hivi watu wa Nigeria wanaingalia timu yao kama yenye uwezo wa kutwaa Kombe la Dunia.
Kwa hiyo kushindwa kufuzu lilikuwa pigo kubwa sana kwao.
Na namna pekee ya wachezaji kuwapoza machungu mashabiki wao ni kutwaa AFCON.
Zaidi ya hapo, Nigeria haijashinda AFCON tangu 2013…wamesubiri sana.
Hata 1980 hawakusubiri namna hii…wakati ule kufuzu tu ilikuwa mafanikio…sasa hivi kufuzu AFCON kwao sio stori tena.
Kwa hiyo hii itakuwa mechi ngumu sana kwa Tanzania.
Matokeo yoyote tutakayopata, tuyapokeaa.
Uganda vs Tanzania – Disemba 27
Sir Alex Ferguson aliwaita Manchester City Noisy Neighbours yaani majirani wenye kelele.
Japo Uganda hawana kelele kubwa sana kwa Tanzania kwa kulingakisha na Kenya, lakini kukutana katika jukwaa kubwa kama AFCON huleta hisia tofauti.
Kelele zitakuwa nyingi na na Afrika Mashariki itachangamka.
Lakini mwisho wa siku hii ndio mechi ambayo watanzania tutawadai wachezaji wetu alama tatu.
Hakuna kisingizio chochote kwa Taifa Stars kutoshinda mechi hii.
Kama alivyosema Mwalimu Nyerere wakati akitangaza vita vya Kagera 1978, kwamba sababu tunayo, nia tunayo na uwezo tunao.
Na kwenye mechi hii ni vile vile, sababu tunayo, nia tunayo na uwezo tunao wa kushinda mechi hii.
Tanzania vs Tunisia- Disemba 30
Wakubwa wengine ambao nao Kombe wamekuwa wakilisikia tu redioni kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Walishinda AFCON 2004 walipoandaa mashindano, na baada ya hapo wamepotea.
Lakini kila wakati wa mashindano hutajwa kama moja ya timu inayopewa nafasi ya kuwa mabibwa.
Hii ni kwa sababu ya ubora wa kikosi chao…kama ilivyo safari hii pia
Kwa hiyo matokeo yoyote tutakayopata hapa yasitushitue sana kama taifa…labda kama tutashinda, au kupoteza kwa mabao meeeeengi sana, hapo sawa.
Lakini sare au kupoteza kwa mabao machache, hiyo ni halali yetu.
Na ikitokea timu yetu ikafuzu kwa hatua ya 16, yatakuwa mafanikio makubwa sana kwetu.
Na wachezaji wetu watakuwa mashujaa waliopitiliza…na watabaki kwenye kumbukumbu maisha yote, na hata kuwavuka wale waliofuzu 1980.
Lakini kama hiyo haiwezekani, basi tupate angalau ushindi wa kwanza.
AFCON 1980 – NIGERIA
Nigeria 3-1 Tanzania
Tanzania 1-2 Misri
Ivory Coast 1-1 Tanzania
AFCON 2019 MISRI
Senegal 2-0 Tanzania
Tanzania 2-3 Kenya
Algeria 3-0 Tanzania
AFCON 2023 IVORY COAST
Morocco 2-0 Tanzania
Tanzania 1-1 Zambia
DRC 0-0 Tanzania
AFCON 2025 MOROCCO
Nigeria vs Tanzania
Tanzania vs Tunisia
Uganda vs Tanzania