Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz alianza kujizolea mashabiki kwa uandishi wake wa kuvutia huku wengi wakimsifu kwa uwezo wake wa kuunganisha Bongo Fleva na Afro pop.

Akiwa na uzoefu wa miaka zaidi ya 10 katika tasnia, tayari ametoa albamu, ameshinda tuzo za ndani na kimataifa na kushiriki katika miradi mingi mikubwa katika tasnia ya muziki. Fahamu zaidi.

1. Jina lake la kisanaa linatokana na jina lake la kuzaliwa la Omary na kisha alipoona ana alama za dimples katika mashavu, ndipo akaunganisha na kupata Ommy Dimpoz, jina linalosimama kama chapa kwa sasa.

2. Dimpoz alianza muziki akiwa Sekondari katika kundi lao walilolipa jina la VIP lililoundwa na watu wanne, kisha akaja kujiunga na Top Band yake TID akiungana na waimbaji wengine akiwemo Steve RnB.

3. Alitoka kimuziki kupitia wimbo wake, Nai Nai (2012) uliyotayarishwa na KTG, huku akimshirikisha Alikiba ambaye walikuja kushirikiana katika nyimbo nyingine kama Kajiandae (2016) na Rockstar (2019).

4. Kufanya vizuri kwa wimbo huo (Nai Nai) kulimwezesha Ommy Dimpoz kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2012 akipokea kijiti hicho kutoka kwa Linah aliyeshinda 2011.

5. Baada ya Ommy Dimpoz waliofuatia kushinda kipengele hicho katika TMA ni Ally Nipishe (2013), Young Killer (2014), Barakah The Prince (2015), Rapcha & Phina (2022) na Chino Kidd 2023.

6. Ziara yake ya kwanza kimuziki (tour) barani Ulaya aliongozana na Alikiba ambaye alikuja kumsaini RockStar Africa wakati huo akiwa miongoni mwa wakurugenzi wa lebo hiyo.

7. Hadi sasa Ommy Dimpoz ametoa albamu moja, Dedication (2022) yenye nyimbo 15, huku ikishirikisha wasanii kama Nandy, Marioo, Musa Keys, Blaq Diamond, Fally Ipupa.

8. Aliaanzisha Poz kwa Poz (PKP) Entertainment, lebo iliyosimamia kazi zake lakini pia ikamsaini Nedy Music aliyetoka kupitia wimbo wake, Usiende Mbali (2016) ambao walishirikiana.

Wimbo huo akafanya vizuri ukikamata chati za vituo vikubwa vya televisheni kimataifa kama MTV Base, Sound City, Trace Urban n.k.

9. Msanii aliyemtoa Ommy Dimpoz chini ya PKP, Nedy Music ndiye mwanamuziki wa kwanza kutokea visiwani Zanzibar kushinda tuzo ya All Africa Music Award (AFRIMA).

10. Baada ya Dimpoz kusainiwa RockStar Africa na baadaye Sony Music Entertainment Africa, huo ukawa mwanzo wa PKP kupotea katika soko la muziki na hatimaye sasa haisikiki tena.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *