Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta, pamoja na wachezaji kadhaa walioko nje ya nchi, wanatarajiwa kujiunga na kambi ya timu hiyo  kuanzia leo huko Cairo, Misri kwa ajili ya  fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizopangwa kuanza Disemba 21 mpaka Januari 18 mwakani.

Ujio wa mshambuliaji huyo hapana shaka unaishusha presha timu hiyo hasa baada ya hivi karibuni kumpoteza Abdul Suleiman ‘Sopu’ ambaye alipata majeraha.

Baadhi ya Wachezaji wa Taifa Stars kwa sasa wapo kambini Cairo chini ya kocha mkuu Miguel Gamondi ambapo baadhi ya wachezaji wameshindwa kuwasili kutokana na majukumu ya timu zao.

Taifa Stars ipo kundi C, pamoja na vigogo Nigeria, Tunisia, pamoja na Uganda.

Mkuu wa msafara wa Taifa Stars, Suleiman Mahmoud Jabir alisema kuwa hadi sasa  mshambuliaji Kelvin John, anayechezea Aalborg BK, alijiunga na kambi siku chache zilizopita, huku kiungo Charles M’Mombwa wa Floriana FC, akiwa naye amejiunga.

Jabir alisema kuwa wachezaji waliobaki  wakiongozwa na Samatta watawasili kuanzia leo, Jumatatu tayari kwa kambi hiyo.

“Kama inavyoruhusiwa na kanuni, wachezaji waliruhusiwa kumalizia mechi zao za ligi na klabu zao mwishoni mwa wiki.  Hivyo kuanzia kesho (leo) tunatarajia wengine kuwasili na kujiunga na kambi,” alisema Jabir.

Alisema kuwa Samatta, anayekipiga kwa Le Havre AC ya Ligue 1 nchini Ufaransa, alikuwa akicheza jana dhidi ya Lyon huku kiungo Novatus Miroshi pia alikuwa na majukumu ya klabu yake ya Göztepe FC ya Ligi Kuu ya Uturuki, ikicheza dhidi ya Gaziantep jana hiyo hiyo.

Wachezaji wengine walioko nje ya nchi wanatarajiwa kujiunga na kambi ni pamoja na beki Haji Mnoga wa Salford City (Uingereza), mshambuliaji Simon Msuva wa Al-Talaba SC (Iraq), kiungo Tarryn Allarakhia wa Rochdale AFC (Uingereza), Miano Danilo wa FK Panevezys (Lithuania), na Alphonse Mabula wa FC Shamakhi ya Azerbaijan.

Tanzania itafungua kampeni yake ya Kundi C dhidi ya Nigeria Desemba 23, kabla ya kukabiliana na Uganda Desemba 27. Taifa Stars kisha itamalizia hatua ya makundi dhidi ya Tunisia Desemba 30.

Juzi usiku, Taifa Stars ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Haras el-Hodoud inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika mchezo huo ambao ni sehemu ya maandalizi ya Taifa Stars kwa ajili ya AFCON 2025, bao pekee la ushindi lilifungwa na Morice Abraham.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *