
Kitengo cha rufani cha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kimetupilia mbali hoja za utawala wa kizayuni wa Israel za kupinga uhalali wa uchunguzi wa mahakama hiyo kuhusu jinai zilizofanywa Ukanda wa Ghaza kufuatia vita vya kinyama na vya mauaji ya kimbari ambavyo utawala huo haramu ulivianzisha Oktoba 7, 2023 dhidi ya Wapalestina wa ukanda uliowekewa mzingiro.
Uamuzi huo ulitolewa jana Jumatatu wakati uchunguzi unaendelea kuhusu jinai na uhalifu wa kivita uliofanywa Palestina ambao umepelekea kutolewa na ICC hati za kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa vita wa zamani Yoav Gallant kwa tuhuma za kuhusika na “uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita” uliofanywa wakati wa vita vya mauaji ya kimbari huko Ghaza.
Utawala wa kizayuni umefanya majaribio kadhaa ya kubatilisha hati hizo za kuwatia nguvuni viongozi wake wakuu, ikiwa ni pamoja na kudai kufanywa upendeleo na mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Karim Khan na kupinga pia mamlaka na uhalali wa mahakama hiyo. Uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuhusu jinai za vita vya Ghaza, ulioanzishwa mwaka 2021 kutokana na ombi la Palestina, hivi karibuni umepanuka kufuatia maombo mengine yaliyotolewa na nchi zingine saba.
Israel ilidai kwamba ilipasa ipokee taarifa rasmi kuhusu uchunguzi mpya unaofanywa dhidi yake kulingana na Kifungu cha 18(1) cha Mkataba wa Roma. Hata hivyo, ICC imetoa uamuzi kwamba uchunguzi wa matukio ya baada ya Oktoba 7 uliingia kwenye notisi ya awali iliyotolewa mwaka2021, na hivyo kubatilisha hitaji la kutolewa taarifa nyingine mpya.
Tangu Oktoba 2023 hadi sasa, jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel limeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 70,400, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine 171,000 katika vita vya miaka miwili dhidi ya Ghaza ambavyo vimeigeuza magofu na vifusi sehemu kubwa ya eneo hilo la ardhi ya Palestina linaloendelea kuzingirwa.
Wataalamu wa sheria wakiwemo wa Umoja wa Mataifa wanasisitiza kuwa utawala ghasibu wa Israel, kwa ushirikiano wa Marekani na mataifa ya Magharibi, umefanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza…/