Tunisia imeitangaza kadhia ya Palestina kuwa ni jeraha kubwa zaidi la mfumo wa haki duniani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia amelitaja suala la Palestina kuwa ni jeraha kubwa zaidi la mfumo wa haki wa kimataifa na kutoa wito wa kuchukuliwa misimamo ya wazi kwa ajili ya kudhaminia haki ya Wapalestina ya kuunda nchi yao huru.
Mohamed Ali Nafti, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia aliyasema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa kuhusu Muungano wa Ustaarabu (UNAOC) uliofanyika Jumamosi na Jumapili tarehe 13 na 14 mwezi huu wa Disemba huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia na kuongeza kuwa: Suala la Palestina ni jeraha kubwa zaidi la mfumo wa haki wa kimataifa. Amesema, mchakato wa muungano huo kuelekea kwenye mazungumzo kati ya tamaduni mbalimbali hauwezi kukamilika bila kushughulikiwa suala la Palestina.
Mkutano wa Riyadh umeshirikisha viongozi wa kisiasa na kidini, wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa, sekta binafsi, asasi za kiraia, wasomi, vijana, wasanii, wanamichezo na wanahabari.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia, Nafti ameashiria mashambulizi yanayoendelea kufanywa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo ya Palestina na kusema: Ukiukaji wa sheria na haki unaoendelea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na mateso yanayowasibu raia vinahitaji msimamo madhubuti na wa wazi wa kimataifa ili kurejesha hadhi kwa sheria za kimataifa za kibinadamu na kudhamini haki za Wapalestina; muhimu zaidi ni kuanzishwa nchi huru ya Palestina, mji mkuu wake ukiwa ni Al Quds Tukufu.
Msimamo wa Tunisia na aghlabu ya nchi za Kiafrika kuhusu kadhia ya Palestina umejengeka katika misingi ya haki, uhuru na kukabiliana na ukoloni. Tunisia imetangaza kuwa suala la Palestina ni jeraha kubwa zaidi la haki katika mfumo wa kimataifa, na bila ya kupatiwa ufumbuzi, hakuna utaratibu wowote wa haki utakaoweza kuundwa. Mtazamo huu umejikita katika historia ya mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi za Magharibi katika nchi za Afrika ambazo zimepitia tajiriba chungu ya ukoloni na ubaguzi.
Tunisia imekuwa ikisisitiza misimamo yake rasmi kuhusu haki ya wananchi wa Palestina kwa ajili ya kuundwa nchi yao huru mji wake mkuu ukiwa Quds. Rais wa Tunisia na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo wameeleza mara kadhaa kwamba kuiunga mkono Palestina si msimamo wa muda, bali ni sera thabiti na ya msingi ya Tunisia. Nchi hiyo pia imelitambua suala la Palestina kuwa kitovu cha kupigania haki katika majukwaa ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na katika mikutano ya Umoja wa Mataifa; na imetaka kurejeshwa haki halali za Wapalestina.
Katika ngazi ya Afrika, nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini, Algeria na Nigeria pia zina misimamo inayoshabihiana kuhusu kadhia hiyo. Afrika Kusini hasa kwa kuzingatia tajiribia ya ubaguzi wa rangi, Apartheid, imezitaja sera za utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Wapalestina kuwa aina ya ubaguzi wa rangi na imekuwa ikilaani sera hizo mara kwa mara. Katika mikutano yao ya pamoja, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia na Afrika Kusini wamesisitiza udharura wa kuendelea kuwaunga mkono na kuwatetea watu wa Palestina na udharura wa kufanyiwa marekebisho miundo ya kimataifa ili kuhakikisha haki inatendeka. Ushirikiano huu unaonyesha kuwa suala la Palestina si daghadagha ya Ulimwengu wa Kiarabu tu, bali pia ni suala muhimu kwa bara zima la Afrika.

Nchi za Kiafrika pia zimepasisha maazimio mbalimbali ya kuiunga mkono na kuitetea Palestina katika Umoja wa Afrika (AU). Msimamo huu umetokana na mshikamano wa kihistoria kati ya mataifa yaliyokoloniwa na watu wa Palestina. Aidha viongozi wengi wa Afrika wanaamini kuwa, ukombozi wa Palestina ni sehemu muhimu ya kupatikana haki duniani.
Kwa ujuma, msimamo wa Tunisia na Afrika kwa ujumla kuhusu kadhia ya Palestina unatokana na uzoefu mchungu wa pamoja wa ukoloni, kupigania haki na uadlifu na kuwepo haja ya kukabiliana na ubaguzi na ukoloni. Nchi hizo zinaamini kuwa kadhia ya Palestina ni mtihani wa kupima ukweli wa madai ya jamii ya kimataifa kuhusu kuheshimu misingi ya uadilifu na haki, na zinaamini kuwa bila ya kutatua mgogoro huo, hakutakuwepo mfumo wa haki duniani.