
Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese ametembelea Hospitali ya St. George kusini mwa Sydney ili kumjulia hali Ahmed Al Ahmed, Mwislamu aliyehatarisha maisha yake kwa kumvamia na kumpokonya bunduki mmoja wa wahusika wa shambulio lililotokea kwenye Ufukwe wa Bondi na kusababisha vifo vya watu 15.
Akiwa amesimama kando ya kitanda cha hospitali alicholazwa Al Ahmed, Albanese amemsifu baba huyo wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 43 kwa ujasiri wake wa ajabu, akimtaja kama nembo ya umoja wa kitaifa katika kukabiliana na ugaidi.
Katika ujumbe alioweka baadaye kwenye mtandao wa kijamii wa X, Waziri Mkuu wa Australia amemhutubu Muislamu huyo: ” Ahmed, wewe ni shujaa wa Australia. Ulijitia hatarini kuwaokoa wengine, ukaikimbilia hatari kwenye Ufukwe wa Bondi na kumpokonya silaha gaidi. Katika nyakati mbaya zaidi, tunawaona Waaustralia walio bora kabisa. Na hivyo ndivyo tulivyoona Jumapili usiku”.
Albanese amemalizia ujumbe wake kwa kusema: “kwa niaba ya kila Muaustralia, nasema ahsante”.
Al Ahmed alijeruhiwa vibaya baada ya kumvamia mmoja wa washambuliaji, akimnyang’anya silaha yake na kumgeuzia, na kumlazimisha mshambuliaji huyo kujisalimisha. Al Ahmed alifyatuliwa risasi mara kadhaa na kupata majeraha kwenye mkono na bega lake. Hata hivyo maafisa wa hospitali wamesema hali yake si mbaya…/