
Mvua kubwa zinazonyesha huko Gaza, zimesababisha mafuriko katika maelfu ya mahema yanayotumiwa na Wapalestina, huku maji yakiingia katika hospitali ya eneo hilo.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Anadolu, maji ya mvua yaliingia sehemu za Hospitali ya Al-Shifa Gaza, hasa maeneo ya mapokezi na kitengo cha dharura, na kuathiri shughuli za hospitali.
Hospitali ya Al-Shifa, kituo kikubwa cha matibabu cha Gaza, imekumbwa na mashambulizi mengi ya Israeli katika kipindi cha miaka miwili ya mauaji ya halaiki na sehemu kubwa kuharibika.
Juhudi za Wizara ya Afya ya Gaza za kurudisha huduma baada ya kusitishwa kwa mapigano hazijafanikiwa kutokana na Israel kuzuia kuingia kwa vifaa vinavyohitajika.
Mashuhuda waliiambia Anadolu kwamba maelfu ya mahema ya watu waliokimbia makazi yameathiriwa na mafuriko na kuangushwa na upepo mkali uliokuwa unavuma katika eneo hilo tangu Jioni ya Jumatatu.
“Tuliamshwa na sauti ya upepo mkali uliogonga hema letu. Tulijaribu kulilinda na kulishikilia, lakini upepo uliangusha hema, na vitu vyetu vyote vilirushwa mbali,’ Khaled Abdel Aziz, Mpalestina aliyekimbia makazi, aliiambia Anadolu.
Mamia ya Wapalestina walijaribu kupata hifadhi dhidi ya mvua chini ya majengo yaliyoharibiwa na jeshi la Israeli Ghaza, kwa mujibu wa mashuhuda.
Wakati huo huo, Mpalestina Maha Abu Jazar alikuwa akikimbia bila mwelekeo pamoja na watoto wake watatu baada ya maji kujaa katika hema lake lililopo mtaa wa Al-Mawasi, magharibi mwa Khan Younis, kusini mwa Gaza.