Tanzania inaendelea kushuhudia ongezeko la watalii kutoka mataifa mbalimbali ya Ulaya, yakiwemo Ufaransa, wanaovutiwa na uzuri wa kipekee wa asili na mandhari tofauti zinazopatikana nchini.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Miongoni mwa vivutio vinavyozidi kuipa Tanzania umaarufu ni hamasa kwa wanandoa wapya wanaotafuta safari za kipekee za fungate. Baadhi ya watalii waliotembelea Tanzania ni wanandoa wapya kutoka Ufaransa, Pauline na Sebastian Clermont-Petit, waliokuja nchini mahsusi kwa ajili ya fungate yao.

Akizungumza na Radio France International (RFI), Pauline alisema wao walichagua Tanzania kwa sababu ilikuwa ndoto yao ya muda mrefu, wakitamani kuanza maisha yao ya ndoa kwa kutengeneza kumbukumbu zisizosahaulika.
Tulifunga ndoa miezi michache iliyopita nchini Ufaransa, na kwa kweli hii ndiyo sehemu bora zaidi kwa fungate. Watu ni wakarimu sana, waongozaji wa watalii wanasaidia mno, na rasilimali za asili ni za kuvutia kupita kiasi.
Sebastian Clermont-Petit alisema kuwa Tanzania ni ya kipekee kutokana na wingi wa wanyamapori wanaopatikana nchini, akitaja hasa wanyama maarufu watano wakubwa (Big Five).

Clermont-petit ambaye ni mpiga picha pia alisema amepata fursa ya kupiga picha nyingi za wanyama ambao hajawahi kuwaona karibu kiasi hicho.
Nimepiga picha nyingi nikiridi nchini kwetu Ufaransa nitakwenda kuwaonyesha wazazi wangu. Sijawahi kuona wanyama wakubwa na wazuri kiasi hiki. Big Five huwezi kuwapata kwa urahisi sehemu nyingine duniani. Chakula pia ni kitamu sana.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Alex Choya, hifadhi imeendelea kuvutia idadi kubwa ya watalii wa kigeni kutokana na umaarufu wake wa kimataifa.
Licha ya matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi, watalii wameendelea kuja, jambo linalowapa uhakika kwamba nchi ipo salama.

Alisema Serengeti ina fursa nyingi za utalii ikiwemo safari za puto, matembezi ya kutembea porini, na matembezi ya usiku yanayoongozwa katika maeneo maalumu, ambayo yote yanavutia idadi kubwa ya watalii.
Tulitaka kusisimka kwa safari za wanyamapori, utulivu wa bahari, na fursa ya kujifunza utamaduni ambao tulikuwa tumeusoma tu kwenye vitabu. Tanzania imezidi matarajio yetu.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waendeshaji Watali Tanzania (TATO), Willy Chambulo, alisema Tanzania inaendelea kujitangaza yenyewe kupitia vivutio vyake vya kipekee.
Sekta ya utalii ya Tanzania imejengwa juu ya rasilimali asilia na wanyamapori. Mlima Kilimanjaro, hifadhi za taifa na wingi wa viumbe hai ndivyo vinavyoifanya Tanzania kuwa ya kipekee duniani.
Kwa wengi, Tanzania imekuwa mwanzo mzuri wa safari ya maisha ya ndoa, wakibeba kumbukumbu zitakazodumu maisha yao yote na hamu ya kurejea tena nchini.