Kamandi ya Kusini ya Jeshi la Marekani imesema imefanya mashambulizi dhidi ya boti tatu katika eneo la kimataifa la Bahari ya Pasifiki, ikidai zilikuwa zikisafirisha madawa ya kulevya. Tukio hilo limesababisha vifo vya watu wanane, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo iliyochapishwa kwenye mtandao wa X.

Jeshi la Marekani linasema taarifa za kijasusi zilithibitisha kuwa boti hizo zilikuwa zikipitia njia zinazojulikana za usafirishaji wa dawa za kulevya katika Bahari ya Pasifiki ya Mashariki. Hata hivyo, hakuna ushahidi wa wazi uliotolewa hadharani kuthibitisha madai hayo.

Mashambulizi hayo ni sehemu ya operesheni kubwa ya kijeshi iliyoanzishwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, dhidi ya biashara ya dawa za kulevya kutoka eneo la Karibiani na Pasifiki. Kwa mujibu wa mamlaka za Marekani, zaidi ya boti 20 zimeharibiwa na takribani watu 90 wanaodaiwa kuwa wasafirishaji wa dawa wameuawa tangu kampeni hiyo ilipoanza mwezi Septemba.

Ukosoaji wa kampeni ya Trump dhidi ya dawa za kulevya

Hatua ya kutumia jeshi kufanya mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya washukiwa wa biashara ya dawa za kulevya imezua mjadala mkubwa, huku baadhi ya wataalamu wa sheria wakisema mashambulizi hayo yanaweza kuchukuliwa kama mauaji haramu nje ya mfumo wa sheria za kimataifa. Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesisitiza kuwa operesheni hizo ni halali chini ya sheria za Marekani na kimataifa.

Mashambulizi hayo yameongeza mvutano kati ya Marekani na Venezuela, huku Washington ikiishutumu serikali ya Rais Nicolas Maduro kwa kuwa na uhusiano na magenge ya biashara ya dawa za kulevya. Serikali ya Venezuela imekanusha madai hayo na kuishutumu Marekani kwa kuandaa mpango wa mabadiliko ya utawala ili kudhibiti rasilimali kubwa za mafuta ya nchi hiyo.

Lukashenko amkaribisha Maduro Belarus, akiamua kuachia madaraka

Ni katika mazingira hayo ambapo Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, amejitokeza kuzungumzia suala la Venezuela, akisema Rais Maduro anakaribishwa nchini Belarus endapo ataamua kuondoka madarakani, ingawa amesema suala hilo halijawahi kujadiliwa rasmi.

“Maduro hakuwa adui wala mpinzani kwetu. Kamwe. Kama angependa kuja Belarus, milango iko wazi,” alisema Rais Lukashenko, na kufafanua kuwa suala hilo halijawahi kujadiliwa.

“Maduro si mtu wa kukimbia. Yeye ni mtu shupavu, kama Chavez. Ni mtu mwenye heshima na ambaye unaweza kukaa naye mezani na kufikia makubaliano,” aliongeza Rais huyo wa Belarus.

Urusi, Kazan 2024 | Mkutano wa Nicolas Maduro na Alexander Lukashenko pembezoni mwa Mkutano wa 16 wa BRICS.
Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko (kulia) amemkaribisha Nicolas Maduro (kushoto), ikiwa ataamua kuachia maraka Venezuela.Picha: Cristian Eloy Torres/TASS/IMAGO

Lukashenko, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema anaamini mgogoro kati ya Marekani na Venezuela unaweza kutatuliwa kwa njia ya amani. Ameonya kuwa vita dhidi ya Venezuela vinaweza kuwa sawa na “Vietnam ya pili” na kusema vitasababisha raia wa Venezuela kumuunga mkono zaidi Rais Maduro.

Kauli za Lukashenko zimekuja wakati Marekani ikiongeza kwa kiwango kikubwa uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Karibiani, hatua inayotafsiriwa na wachambuzi kama maandalizi ya mashambulizi ya ardhini ambayo Rais Trump amesema yanaweza kuanza hivi karibuni.

Wakati mjadala huo ukiendelea, shinikizo linaongezeka ndani ya Bunge la Marekani, ambapo maafisa wakuu wa serikali wanatarajiwa kutoa maelezo ya kina kuhusu uhalali na malengo ya operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa biashara ya dawa za kulevya.

Chanzo: retre, afpe, ape

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *