Bunge nchini Zambia limepitisha kwa sauti moja muswaada wa kubadili vifungu kadhaa vya katiba vinavyohusiana hasa na sheria za uchaguzi, huku upinzani ukilalamika kwamba hatua hiyo ni mpango wa kuimarisha nafasi ya rais Hakainde Hichilema katika uchaguzi ujao.
Zambia inatarajia kuingia kwenye uchaguzi mwezi Agosti mwaka ujao lakini tayari upinzani unahisi zipo njama za kumuimarisha rais Hakainde Hichilema kushinda kirahisi uchaguzi huo.
Wanasiasa wa upinzani mashirika ya kiraia na makanisa kadhaa yamekuwa yakifanya kampeni ya kupinga muswaada wa kuifanyia marekebisho katiba wakisema muswaada huo umepitishwa harakaharaka bungeni na lengo lake ni kumpa nguvu Hichilema na chama chake cha UPND katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Mwandishi wa habari Mary Kimiti aliyeko Zambia ameiambia Dw kwamba anaamini muswaada huo sio tu umepitishwa na wabunge kwa kishindo lakini inaonesha unaungwa pia mkono na Wazambia wenyewe.
Muswaada uliopitishwa unapendekeza mabadiliko ya vipengele kiasi 13 vya katiba ikiwa ni pamoja na kupendekeza kuongezwa idadi ya wabunge wa kuchaguliwa kutoka viti 156 hadi 226, na kutenga nafasi maalum kwa wanawake.
Waziri wa sheria wa Zambia Princess Kasune amesema kupitishwa kwa muswaada huo na idadi ya wabunge 131 dhidi ya 2 walioupinga inaonesha ni hatua ya agano la ahadi na wananchi wa Zambia la kuimarisha hali ya usawa kwenye taifa hilo la Kusini mwa Afrika. Wazambia wapiga kura katika uchaguzi wa rais
Hata hivyo mbunge wa chama cha upinzani cha Patriotic Front PF Francis Kapyanga amesema hayuko tayari kuona haramu inahalalishwa.
Rais Hakainde Hichilema sasa anasubiriwa kuudhinisha muswaada huo kuwa sheria kamili huku mivutano ya kisiasa katika taifa hilo la wakaazi milioni 22 ikiendelea kuonekana waziwazi hasa baada ya mkwamo uliotokana na maziko ya mtangulizi wa Hichilema, Edgar Lungu aliyefariki nchini Afrika Kusini mnamo mwezi Juni.
Wazambia wanashiriki katika uchaguzi wa rais na Bunge Msemaji wa familia ya Lungu ambaye pia ni mgombea anayetarajiwa kuwania urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha PF Makebi Zulu amesema kupitia ujumbe aliyouandika kwenye mtandao wa kijamii kwamba hatua iliyochukuliwa na bunge inaanzisha mapambano ya kudai demokrasia na kuheshimiwa utawala wa sheria nchini Zambia.
Rais Hichilema mwenyewe amekiri kwamba muswaada huo umeonesha kupima mshikamano wa taifa lakini hatua iliyopitishwa na bunge inapaswa kuheshimiwa.