Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) waliokutano huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria, wamelaani wimbi la mapinduzi ya kijeshi katika eneo hilo na kukubaliana kuunda kikosi cha pamoja cha kuchukua hatua za mapema za kukomesha mapinduzi na ukosefu wa usalama.

Katika mkutano huo, nchi wanachama wa ECOWAS zimekubaliana kuelekea kwenye hatua za kuchukua hatua za kuzuia migogoro kama vile hatua za mapema kijeshi na uingiliaji kati wa kidiplomasia, badala ya kuchukua hatua baada ya tukio, kama kuweka vikwazo. Pia wameelezea masikitiko yao kutokana na kuongezeka ugaidi na ukosefu wa usalama katika eneo hilo na wamekubali kuchukua hatua za pamoja kushughulikia vitisho hivyo.

Ingawa bara la Afrika linakabiliwa na matatizo mengi ya kisiasa na kiuchumi kwa miongo kadhaa, ikiwa ni pamoja na mapinduzi ya kijeshi, watawala wa kidikteta, uhaba wa chakula na uwepo wa makundi ya kigaidi, lakini matatizo haya yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Katika suala hili, udhaifu wa taasisi za serikali, matatizo ya kiuchumi, vitisho vya kigaidi, ushawishi hasi wa nchi za kigeni na sifa maalumu za kijiografia za eneo hilo, vyote vimechangia kutengeneza mazingira ya kuongezeka migogoro na ukosefu wa amani katika nchi za Afrika Magharibi, kiasi kwamba nchi zilizo zimeshuhudia wimbi la mapinduzi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni, ambayo yameathiri vibaya utulivu wa kisiasa na kiuchumi wa eneo hilo.

Mojawapo ya sababu kuu za mapinduzi ya kijeshi Afrika Magharibi ni udhaifu wa serikali za kidemokrasia na taasisi za serikali. Nchi nyingi katika eneo hilo zinakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, ufisadi na kutoweza kutoa huduma za kutosha za umma. Taasisi za serikali katika nchi mbalimbali za Magharibi mwa Afrika, ikiwa ni pamoja na Guinea-Bissau, Mali na Niger, zimeshindwa kukidhi matarajio ya watu na kudhibiti migogoro ya kiuchumi na kijamii. Suala hili limesababisha hali ya kutoridhika miongoni mwa umma na hata katika baadhi ya vikosi vya jeshi, jambo ambalo limechochea mapinduzi mengi.

Viongozi wa kijeshi wa Mali, Niger na Burkina Faso

Kwa upande mwingine, dalili za uingiliaji kati wa kigeni zinaonekana wazi katika nchi nyingi za Magharibi mwa Afrika. Kuwepo rasilimali nyingi za asili na nishati, pamoja na eneo maalumu la kijiografia, kumekuwa sababu ya kuendelea uingiliaji kati wa nchi za kigeni katika nchi nyingi za eneo hilo kiasi kwamba, rasilimali na matakwa ya nchi hizo yameathiriwa na sera na malengo ya nchi za Magharibi. Hali ya kisiasa katika baadhi ya nchi za eneo hilo pia imesababisha mifumo wa kisiasa ya nchi kuendelea kuwa ya kidikteta, licha ya madai kwamba ni ya kidemokrasia. Katika baadhi ya nchi hizo, viongozi walioko madarakani wamebadili sheria na katiba ili kuendelea kuwa madarakani, suala ambalo limeibua upinzani mkubwa na kutayarisha mazingira ya mapinduzi ya kijeshi.

Kwa upande mwingine, Afrika Magharibi imekuwa ikikabiliwa na ongezeko na ustawi wa makundi ya kigaidi na yenye msimamo mkali, hasa katika muongo mmoja uliopita. Harakati za makundi hayo zimezifanya serikali za nchi nyingi za Magharibi mwa Afrika zishindwe kulinda usalama wa ndani na katika mipaka yao.

Kwa mtazamo mwingine, mapinduzi ya kijeshi huko Afrika Magharibi si tishio kwa demokrasia tu, bali pia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa upande mmoja, matukio hayo yanapelekea kudhoofika imani ya umma kwa taasisi za serikali na michakato ya kidemokrasia, na kwa upande mwingine, yanaeneza hofu ya ukosefu wa utulivu wa kiuchumi katika ngazi za ndani na kimataifa. Hali hii imepunguza uwekezaji wa kigeni, kuvuruga biashara na shughuli za kiuchumi na kusababisha kupungua kwa ustawi wa uchumi, mambo ambayo yamezidisha ongezeko la ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei.

Wananchi Niger

Katika hali hii, ECOWAS, kama mojawapo ya taasisi muhimu za kikanda huko Magharibi mwa Afrika, inajaribu kuzuia kuenea kwa mapinduzi ya kijeshi na ukosefu wa usalama kupitia hatua mbalimbali. Ili kukabiliana na wimbi la mapinduzi la hivi karibuni, jumuiya hiyo imeamua kutumia mbinu mpya inayozingatia zaidi kuchukua hatua mapema na za kuzuia, badala ya mwenendo wa hapo awali wa kushughulia migogoro iliyokwisha tokea. Katika mkutano wa Abuja, wakuu wa nchi wanachama wa ECOWAS wametangaza rasmi kwamba, badala ya kuweka vikwazo vya kiuchumi na kidiplomasia, ambavyo vimekuwa na mafanikio madogo katika kukabiliana na masuala kama mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara, watachukua hatua kama vile uingiliaji kati wa kijeshi na kuzihami serikali halali. Kwa hakika, ECOWAS inafanya jitihada za kuimarisha utulivu na amani ndelevu katika eneo la Afrika Magharibi kwa kutumia mikakati hiyo mipya.

Wanachama wa ECOWAS pia wanatumai kwamba kwa kudumisha mshikamano miongoni mwa nchi wanachama, wataweza kuiondoa kanda hiyo kwenye mtego wa migogoro ya muda mrefu na kuzuia mapinduzi zaidi ya kijeshi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *