Leo ni Jumatano tarehe 26 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria mwafaka na tarehe 17 Disemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi.
Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Muhammad (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waende kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea Madina.
Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea bila mafanikio. Wakati huo Mtume (saw) alimteua Ali bin Abi Twalib (a.s) kuongoza jeshi la Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi.
Wafasiri na wanahistoria wengi wamehusisha kuteremshwa Suratul-A’diyat na vita hivi muhimu na vilivyoambatana na ushindi.

Miaka 247 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Humphrey Davy mwanakemia na mwanafikizia wa Kiingereza.
Katika majaribio yake ya kimaabara, msomi huyo aliweza kutenganisha elementi za Sodium, Potassium, Calcium, Barium, Magnesium na Strontium miongoni mwa elementi nyinginezo na hatua hiyo ilihesabiwa katika zama hizo kuwa mafanikio makubwa katika sayansi ya kemia.
Davy mbali na kuwa mwasisi wa elimu inayojulikana kama “electrochemical”, aliweza pia kuwasilisha nadharia ambayo iliitaja gesi ya Hydrojen kuwa gesi inayoweza kuzitambua asidi. Mwanakemia huyo wa Kiingereza alifariki dunia mwaka 1829.

Katika siku kama ya leo miaka 122 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Disemba mwaka 1903, ndege ya kwanza duniani iliyokuwa ikitumia injini ya mota, ilifanikiwa kuruka na kupaa angani kwa dakika moja baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa.
Ndege hiyo ilitengenezwa na ndugu wawili walioitwa Wilbur na Orville Wrights na kufanyiwa majaribio katika jimbo la North Carolina nchini Marekani.
Ndugu hao wawili walikuwa watengeneza baiskeli ambao baadaye walipatwa na shauku kubwa ya kutengeneza ndege yenye kutumia injini ya mota.

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo mwili wa Mhandisi Muhammad Javad Tondguyan, Waziri wa Mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ulirejeshwa nchini kutoka Iraq baada ya kupita miaka 11.
Waziri Tondguyan na maafisa wengine kadhaa wa wizara hiyo walitekwa nyara na wanajeshi wavamizi wa Iraq wakati walipokuwa katika ziara ya kutembelea visima vya mafuta vya kusini mwa Iran. Waziri huyo na wenzake walitekwa nyara mwezi mmoja baada ya Iraq kuvamia ardhi ya Iran.
Utawala wa Saddam wakati huo uliendelea kukanusha kutekwa nyara Mhandisi Tondguyan kwa muda fulani, lakini hatimaye ulikiri kumteka nyara waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran.
Uchunguzi wa kidaktari na ushahidi uliotolewa na watu waliokuwa karibu na Waziri Muhammad Jawad Tondguyan ulithibitisha kwamba waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran alikufa shahidi kutokana na kuteswa na askari jeshi wa utawala wa Baath wa Iraq.

Tarehe 17 Disemba mwaka 1992 yaani siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kisingizio cha kuuawa polisi wake mmoja wa mpakani, uliwabaidisha kusini mwa Lebanon viongozi 415 wa harakati ya Jihadul Islam na Hamas kutoka Palestina.
Baada ya serikali ya Lebanon kupinga hatua hiyo isiyo ya kibinadamu na kukataa kuwapokea Wapalestina hao, hasira na upinzani wa ulimwengu wa Kiislamu ulilifanya Baraza la Usalama kupitisha azimio nambari 977 lililolaani hatua hiyo ya Tel Aviv na kutaka kurejeshwa Wapalestina hao waliobaidishwa nchini kwao.

Na siku kama hii ya leo tarehe 17 Disemba miaka 15 iliyopita kijana mmoja wa Kitunisia aliyejulikana kwa jina la Tariq Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliotawala kwa kipindi cha nusu karne.
Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.
Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya Chuo Kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyanganywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa halmashauri ya mji na ndipo alipoamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin.
