
SI uliona ushindani wa wachezaji ulivyokuwa msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara na mwisho wa yote wale wa kigeni walitawala sehemu kubwa mbele ya wazawa? Ngoma ya msimu huu imeanza kwa kasi ya ajabu, huku wazawa wakiamka.
Msimu uliopita kinara wa mabao alikuwa mchezaji wa kigeni, Jean Charles Ahoua, raia wa Ivory Coast, anayecheza Simba aliyefunga mabao 16, akifuatiwa na mzawa Clement Mzize (14), kisha wageni wakafuatia ambao ni Mghana Jonathan Sowah (13), Mganda Steven Mukwala (13), Mghana Leonel Ateba (13), Mzimbabwe Prince Dube (13), Muivory Coast Pacome Zouzoua (12), Mgambia Gibril Sillah (11), Mkenya Elvis Rupia 10) na Mbukinabe Stephane Aziz (9).
Upande wa clean sheet alikuwa kipa wa kigeni anayeitumikia Simba, Moussa Camara raia wa Guinea aliyemaliza na 19. Alifuatiwa na mgeni mwingine, Mmali Djigui Diarra wa Yanga (17). Wazawa Patrick Munthali (12) na Yona Amosi (11) wakafuatia.
Katika asisti, mzawa Feisal Salum wa Azam aliongoza na 13, chini yake kukawa na wageni ambao ni Mkongomani Maxi Nzengeli (10), Muivory Coast Pacome Zouzoua (10), Muivory Coast Jean Charles Ahoua (9), Mzimbabwe Prince Dube (8), Muivory Coast Josephat Bada (8), Mbukinabe Stephane Aziz KI (7) na Mkongomani Elie Mpanzu (6).
Kwa muda mrefu, wachezaji wa kigeni wamekuwa wakitawala kitakwimu ndani ya Ligi Kuu Bara lakini msimu huu hadi sasa, kuna mabadiliko makubwa licha ya kwamba kuna viporo vingi vya mechi ambavyo vinaweza kubadilisha upepo.
Wakati hayo yakijiri, juzi Jumapili, zilipigwa mechi mbili ambazo ni za mwisho kwa mwaka huu 2025, kisha Ligi Kuu Bara imesimama kupisha Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025) zitakazoanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.
Wakati ligi ikisimama JKT Tanzania ikiwa kileleni mwa msimamo ikikusanya pointi 17 ikicheza mechi 10, inafuatiwa na Yanga yenye pointi 16 zilizotokana na mechi sita ilizocheza.
Ligi hiyo imesimama zikiwa zimepigwa mechi 62, huku yakipatikana mabao 104. Katika mabao hayo, wageni wamefunga 37, wazawa 60, huku manne ya kujifunga na matatu ya mezani waliyopata Pamba Jiji dhidi ya Dodoma Jiji kufuatia mechi yao kutochezwa kutokana na mwenyeji Dodoma Jiji kuonekana kushindwa kuandaa mchezo.
Katika orodha ya wafungaji yakiwa yamepatikana mabao 104 katika mechi 62, kinara wa jumla ni mzawa, Paul Peter anayecheza JKT Tanzania mwenye mabao matano, anayefuatia pia ni mzawa, Saleh Karabaka naye anakipiga JKT Tanzania, amefunga manne.
Mchezaji wa kigeni mwenye mabao mengi ni Mganda Peter Lwasa wa Pamba Jiji mwenye matatu sawa na Mkongomani Fabrice Ngoye na Mghana Jonathan Sowah.
Kinara wa msimu uliopita, Jean Charles Ahoua, raia wa Ivory Coast amefunga bao moja, huku Clement Mzize aliyekuwa kinara upande wa wazawa, bado hajafunga kwani muda mrefu yupo nje akiuguza majeraha wakati kikosi anachokitumikia cha Yanga kikishuka dimbani mara sita.
WALIOJIFUNGA
Nyota wanne wamejifunga kwa nyakati tofauti walipokuwa kwenye harakati za kuokoa hatari. Mabao hayo manne ya kujifunga, yamechangia kufikisha idadi ya mabao 104 yaliyopatikana kwenye ligi hadi sasa.
Katika mabao hayo manne ya kujifunga, wazawa wamechangia matatu na moja kutoka kwa mchezaji wa kigeni.
Wazawa waliojifunga ni Haroub Abdallah wa Coastal Union katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji, nyota wa Fountain Gate Lamela Maneno mechi dhidi ya Mtibwa Sugar na Ibrahim Nindi wa KMC alifanya hivyo dhidi ya JKT Tanzania.
Kwa upande wa nyota wa kigenj, Muivory Coast, Anthony Tra Bi Tra wa Singida BS alifanya hivyo dhidi ya TRA United.
Jumla ya penalti nane zimepigwa, ikishuhudiwa sita zikitikisa nyavu na mbili wapigaji wakikosa baada ya makipa kuzicheza.
Katika penalti hizo, wazawa wamepiga tano, wamefunga tatu na kukosa mbili. Waliofunga ni Habib Kyombo wa Mbeya City dhidi ya Fountain Gate, Idd Kipagwile wa Dodoma Jiji dhidi ya TRA United na Maabad Maulid wa Coastal Union dhidi ya Mbeya City.
Waliokosa ni Athuman Makambo wa Coastal Union dhidi ya Fountain Gate na Lucas Kikoti wa Namungo dhidi ya Azam.
Wageni watatu waliopiga na kutikisa nyavu ni Andy Boyeli wa Yanga dhidi ya KMC, Prince Dube wa Yanga dhidi ya Fountain Gate na Clatous Chama wa Singida Black Stars dhidi ya TRA United.
Ukiachana na vita ya ufungaji ilivyokuwa kali msimu uliopita, mtifuano mwingine ulikuwa katika kutengeneza mabao (asisti) ambapo mzawa Feisal Salum wa Azam alikuwa kinara akimaliza na 13.
Msimu huu hadi sasa, kinara pia ni mzawa Andrew Chamungu wa Namungo mwenye tatu. Chini yake ndio kuna mchanganyiko wa wazawa na wageni wakiwa na mbili, huku listi ya wenye moja ni ndefu sana.
Abdi Banda wa Dodoma Jiji, Hassan Kibailo (Pamba Jiji), Ally Ng’anzi (TRA United) na Nassor Saadun (Azam) ni wazawa wenye asisti mbili kila mmoja.
Kinara wa asisti upande wa wageni ni Mkongomani Maxi Nzengeli wa Yanga mwenye mbili sawa na Muivory Coast Pacome Zouzoua (Yanga), Mkenya Mathew Momanyi (Pamba Jiji), Mghana Ibrahim Imoro (Mtibwa Sugar), Mkongomani Ellie Mpanzu (Simba) na Mkenya Duke Abuya (Yanga).
CLEAN SHEET
Kati ya zile vita tatu kubwa za wachezaji kwenye ligi, ishu ya clean sheet nayo imo ambapo tumeshuhudia katika misimu minne mfululuzo, makipa wa kigeni wakitawala.
Msimu wa 2021-2022 na 2022-2023 alikuwa Djigui Diarra wa Yanga raia wa Mali, kisha 2023-2024 alikuwa Mkongomani Ley Matampi aliyekuwa Coastal Union na msimu uliopita 2024-2025 ilikuwa zamu ya kipa wa Simba, Moussa Camara raia wa Guinea ambaye msimu huu anayo moja, amekaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti.
Msimu huu, kipa mzawa wa Mashujaa, Erick Johola anaongoza akiwa nazo sita, wanaofuatia pia ni wazawa Omar Gonzo wa JKT Tanzania mwenye nne sawa na Constantine Malimi wa Mtibwa Sugar.
Kipa wa kigeni mwenye clean sheet nyingi ni Mgabon Jean-Noël Amonome wa TRA United mwenye tatu sawa na Mmali Diarra Djigui (Yanga) na Mnigeria Amas Obasogie (Singida Black Stars).
Clean sheet hizo tatu pia ni sawa na makipa wazawa sita. Beno Kakolanya (Mbeya City), Rashid Ibrahim Abdallah (Fountain Gate), Ally Salim (Dodoma Jiji), Wilbol Maseke (Coastal Union), Yakoub Suleiman (Simba) na Yona Amos (Pamba Jiji).
KADI NYEKUNDU
Katika mechi 62, kadi nyekundu zimeonyeshwa saba, wazawa wakiwa nazo sita na moja ikienda kwa nyota wa kigeni.
Wazawa waliokumbana na adhabu hiyo ni Lucas Kikoti wa Namungo, Haroub Abdallah (Coastal Union), Ramadhan Chalamanda (JKT Tanzania), Mohammed Mussa Salum (Mashujaa), Hamis Mgunya (Namungo) na Vitalis Mayanga (Mbeya City).
Mcolombia Fuentes Mendoza wa Azam, ndiye nyota wa kigeni pekee hadi sasa aliyeonyeshwa kadi nyekundu.