
Baraza hilo lilikubaliana mjini The Hague, Uholanzi, siku ya Jumanne (Disemba 16) kuanzisha kile kinachoitwa Kamisheni ya Kimataifa ya Madai, kama sehemu ya mfumo wa fidia.
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliyehudhuria mkutano huo aliwashukuru washiriki kwa uungaji mkono wao kwa nchi yake.
Makubaliano ya kuanzisha kamisheni hiyo yalisainiwa na mataifa 34, ikiwemo Ujerumani na pia Umoja wa Ulaya. Mataifa na mashirika yaliyo nje ya Ulaya yanaweza pia kujiunga na mpango huo, kwa mujibu wa makubaliano hayo.
Kamisheni hiyo imepewa jukumu la kutathmini madai ya fidia kutoka kwa raia wa kawaida, jumuiya na mashirika ya umma yaliyoathirika na uvunjaji wa sheria za kimataifa uliofanywa na Urusi, na kisha kuamua kiwango cha fidia kinachopaswa kulipwa.