
Kwa mujibu wa barua ya wizara ya mambo ya kigeni ya Venezuela iliyochapishwa jana, Caracas inautaka Umoja wa Mataifa kulaani uharamia huo unaofanywa na Marekani, matumizi ya nguvu za kijeshi yasiyo halali dhidi ya vyombo vya baharini, na wizi wa mzigo ulio kwenye safari halali kimataifa.
Venezuela imetaka pia kuachiliwa mara moja kwa mabaharia wake wanaoshikiliwa na Marekani. Barua hiyo iliwasilishwa kwa rais wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mwanadiplomasia Samuel Zbogar wa Slovenia.
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amedai kuwa hatua ya Marekani kutuma kiwango kikubwa cha wanajeshi karibu sana na nchi yake ni sehemu ya mpango wa kumuondowa madarakani na kuiba akiba kubwa ya mafuta kwa kisingizio cha vita dhidi ya madawa ya kulevya.