
Licha ya makubaliano hayo kusainiwa mapema mwezi Desemba, eneo la Kongo Mashariki linasalia kuwa uwanja wa mapigano. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu laki tano walilazimika kuyahama makazi yao katika wiki moja tu baada ya makubaliano hayo. Mashirika ya misaada yanasema badala ya kuleta utulivu, makubaliano hayo yalichochea mapigano mapya,na kusababisha waasi wa M23 kutwaa maeneo zaidi, ikiwemo mji wa Uvira.
Na DRC siyo mfano pekee. Baada ya sherehe za amani zilizoandaliwa na White House mwezi Oktoba, zaidi ya watu nusu milioni walikimbia mapigano mapya ya mpakani kati ya Thailand na Cambodia. Aidha, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas yameripotiwa kukiukwa mara kadhaa.
Wachambuzi wanasema katika baadhi ya matukio, Trump amekuwa akitangaza kumaliza migogoro ambayo haikuwa vita kamili, bali ilikuwa tofauti za kidiplomasia. Kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa, Theo Zenou, juhudi za Trump zinaendeshwa zaidi na tamaa ya sifa kuliko ujenzi wa amani ya kudumu.
“Trump anaongozwa na tamaa ya kutambuliwa kimataifa kama kiongozi mkubwa. Anataka aonekane kama mleta amani, lakini hataki kufanya kazi ngumu ya kusimamia mazungumzo marefu ya maridhiano. Badala yake, anatafuta ushindi wa haraka na picha za kamera ili kudai amefanikisha amani.”
Lakini kuna sababu nyingine nyuma ya diplomasia hii — ushindani wa ushawishi wa dunia, hasa dhidi ya China. Mtafiti Eugenio Costa Almeida anasema Marekani inatumia makubaliano haya kujionyesha kama mpatanishi muhimu duniani, hasa wakati China inaongeza ushawishi wake barani Afrika.
“Diplomasia ya Trump inalenga kuonyesha uongozi wa kimataifa wa Marekani, hasa wakati China inaongeza ushawishi wake Afrika. Ushindani wa rasilimali muhimu, kama madini ya DRC, unaweza kuwa sababu iliyojificha nyuma ya juhudi hizi za amani.”
Kwa wakosoaji, mikataba hii ya amani ni zaidi ya kauli za kisiasa kuliko suluhisho la kudumu. Wanasema mara nyingi huahirisha migogoro badala ya kuimaliza. Kwa hivyo, licha ya kauli za ushindi kutoka Ikulu ya Marekani, White House, wachambuzi wanaonya kuwa si kila kinachoitwa amani ni amani ya kweli.