
WAKATI dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Januari Mosi, 2026 uongozi wa Mbeya City uko katika mazungumzo ya kuipata saini ya kiungo wa Namungo, Abdallah Mfuko ikiwa ni pendekezo pia la kocha mkuu mpya, Mecky Maxime.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo zimeeleza, Mfuko anayeweza kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani, ni miongoni mwa nyota wanaohitajika na Maxime kutokana na uhusiano mzuri waliokuwa nao wakati wakiwa wote Kagera Sugar.
Mfuko na Maxime wamefanya kazi pamoja wakiwa Kagera Sugar, kabla ya mchezaji huyo kuondoka na kujiunga na Wauaji wa Kusini, yaani Namungo, ambako hadi sasa amebakisha mkataba wa miezi sita unaofikia tamati mwisho wa msimu huu.
“Tunaamini uhusiano mzuri kati ya mchezaji na kocha unaweza kurahisisha kumpata kwa sababu amebakisha miezi sita na waajiri wake Namungo, japo hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa baina ya klabu mbili,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, licha ya mazungumzo hayo ya nyota huyo kujiunga na Mbeya City iliyorejea tena Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, itakutana na ushindani pia baada ya mabosi wa TRA United kudaiwa kuanza kumnyemelea.
Mfuko alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Namungo akitokea Kagera inayocheza kwa sasa Ligi ya Championship, ambao unaisha mwishoni mwa msimu huu, jambo linaloziingiza vitani timu mbalimbali kuanza kuifuatilia huduma yake.
Maxime aliyechukua mikoba ya Malale Hamsini aliyejiunga na KVZ ya Zanzibar, inaelezwa amemsajili kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana.