
MSHAMBULIAJI chipukizi wa Kitanzania, Morice Sichone amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Gulf FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza huko United Arab Emirates akitokea Tridents FC ya Zambia.
Ikumbukwe hivi karibuni kinda huyo alikuwa na mgogoro na chama lake la zamani Tridents ambao hawakuwa tayari kumuachia kwenda Namungo ya Tanzania ambayo ilitajwa kumsajili licha ya kubakiza miezi miwili ya mkataba.
Akizungumza baada ya kukamilisha usajili huo, mshambuliaji huyo amesema lengo lake la kwanza ni kufanya vizuri ndani ya klabu hiyo mpya ili kujijengea heshima na nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.
“Nimekuja hapa kufanya kazi kwa bidii na kuisaidia timu kufikia malengo yake kama ambavyo umekuwa ukifahamu nimekuwa nje ya uwanja muda mrefu, natamani kurudi taratibu na niweze kuonyesha kiwango changu,” amesema Sichone.
“Sikuwa na msimu mzuri, nimekumbwa na majeraha yaliyoniweka nje muda mrefu kidogo, mbaya zaidi sehemu yenyewe niliyokuwa nimeumia ni ndogo, pia ishu ya mgogoro na klabu, lakini nashukuru Mungu mambo yako sawa na naamini nitarudi taratibu.”
Mbali na malengo ya klabu, Sichone ameweka wazi ndoto yake kubwa zaidi ni kuichezea tena timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 na hilo litampa jukwaa la kuonekana zaidi na makocha wa timu za taifa.
“Ndoto yangu ni kuendelea kuivaa jezi ya taifa. Hii ni hatua ya kunisogeza karibu na lengo hilo na naamini bado kijana mdogo nikipambana nafasi ipo,” aliongeza.
Hatua ya kusaini Ligi ya Daraja la Kwanza UAE inatajwa kuwa ni changamoto mpya kwake, hasa ukizingatia kasi na miundombinu ya soka la Mashariki ya Kati. Hata hivyo, alisisitiza kuwa yupo tayari kukabiliana na ushindani huo na kuonyesha uwezo wake.
Kwa upande wa Gulf FC, ujio wa Sichone unatarajiwa kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji, hasa katika kipindi hiki ambacho timu hiyo inalenga kufanya vizuri na kupanda daraja, wakiamini mshambuliaji huyo anaweza kuwa silaha muhimu msimu huu.