
Waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa, serikali yake imeidhinisha makubaliano makubwa ya uuzaji wa gesi asilia kwa Misri yenye thamani ya karibu dola bilioni 35, akielezea kwamba makubaliano hayo ni makubwa zaidi katika historia ya Israel kwa upande wa thamani na ujazo wa usafirishaji nje.
Chaneli 14 ya Israel imemnukuu Netanyahu akisema kwamba, makubaliano ya gesi na Misri yanawakilisha “mafanikio ya kiuchumi na kimkakati”.
Chini ya makubaliano hayo, gesi asilia itasafirishwa kutoka vitalu vya gesi vinavyokaliwa kwa mabavu na utawala wa kizayuni, hususan kitalu cha Leviathan hadi Misri kwa muda wa miaka mingi na kwa viwango vikubwa.
Hii inaashiria mabadiliko ya wazi kutoka miaka iliyopita, wakati Misri ilipowahi kufikia hatua ya kujitosheleza kwa gesi asilia na hata kuweza baadhi ya wakati kusafirisha kwa kuuza nje ya nchi.
Licha ya tangazo hilo lililotolewaa na utawala wa kizayuni kupitia waziri mkuu wake, serikali ya Misri bado haijatoa taarifa yoyote rasmi inayothibitisha maelezo ya makubaliano hayo au kuelezea masharti yake, ikiwa ni pamoja na bei, ujazo, muda wa mkataba, au mifumo ya utekelezaji.
Baadhi ya wadadisi wa mambo wanasema, tangazo la upande mmoja lililotolewa na Israel linaonyesha uhasasi na unyeti ulioko ndani ya Misri juu ya suala hilo, huku kukishuhudiwa mijadala ya mara kwa mara ya umma kuhusu uagizaji wa gesi kutoka Israel na athari zake hasi kwa usalama wa nishati wa Misri pamoja na uhuru na kujitawala kiuchumi nchi hiyo…/