
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International tawi la India, vyama vya siasa vya upinzani na wanaharakati mbali mbali wa ndani na nje ya nchi hiyo wamelaani vikali kitendo alichofanya Waziri Kiongozi wa Jimbo la Bihar cha kumvua niqabu hadharani daktari Muislamu katika hafla ya kiserikali iliyofanyika katika jimbo hilo.
Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii inamuonyesha waziri kiongozi wa jimbo la Bihar, Nitish Kumar akikivuta hadi chini ya kidevu kitambaa cha niqabu alichokuwa amevaa usoni daktari Nusrat Parveen wakati alipoelekea jukwaani kukabidhiwa barua yake ya uteuzi.
Katika video hiyo inayohusiana na hafla iliyofanyika siku ya Jumatatu, Kumar anaonekana kwanza akimpa ishara Bi Nusrat Parveen akivue kitambaa hicho, lakini ghafla yeye mwenyewe akachukua hatua ya kukishusha chini ghafla. Naibu waziri kiongozi wa jimbo hilo la Bihar, Samrat Choudhary, ambaye alikuwa amesimama nyuma ya Kumar, anaonekana kuingilia kati kujaribu kumzuia asifanye hivyo, huku waziri wa afya Mangal Pandey na katibu mkuu wa waziri huyo kiongozi, Deepak Kumar, wanaonekana wakicheka.
Aakar Patel, Mwenyekiti wa Bodi katika Amnesty International nchini India amesema: “kitendo hiki ni shambulio dhidi ya heshima, uhuru, na utambulisho wa mwanamke huyu. Afisa wa umma anapovua hijabu ya mwanamke kwa nguvu, hutuma ujumbe kwa umma kwa ujumla kwamba tabia hii inakubalika. Hakuna mtu mwenye haki ya kudhibiti imani au mavazi ya mwanamke”.
Patel ameendelea kueleza: “vitendo kama hivi vinaongeza hofu, vinaufanya ubaguzi uonekane jambo la kawaida, na vinaharibu misingi ya usawa na uhuru wa kidini. Ukiukaji huu unahitaji kulaaniwa vikali na kuwajibishwa. Hatua za haraka lazima zichukuliwe ili kuhakikisha kwamba hakuna mwanamke anayetendewa vibaya kama hivyo.”
Chama kikuu cha upinzani nchini India cha Congress kimekielezea kitendo cha Kumar kuwa ni kitu “kiovu” na kusisitiza kwamba waziri kiongozi huyo wa jimbo la Bihar anapaswa ajiuzulu wadhifa wake, huku chama cha RJD chenye makao yake makuu kwenye jimbo hilo la Bihar kikitilia shaka utimamu wa akili wa kiongozi huyo na kusisitiza kwamba huo unaweza ukawa uthibitisho wa kuzorota afya yake ya akili…/