
KLABU ya Simba, leo Ijumaa, Desemba 19, 2025 imemtangaza Steve Barker kutoka Afrika Kusini kuwa Kocha Mkuu mpya.
Barker (57), anajiunga na Simba akitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini aliyoiongoza kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
Katika msimu huu, Barker ambaye alizaliwa nchini Lesotho, ameiongoza Stellenbosch katika mechi 24 za mashindano tofauti.
Timu hiyo katika mechi hizo 24, imepata ushindi mara nane, sare sita na kupoteza kumi.
Kabla ya kuiongoza Stellenbosch, Barker alizifundisha pia Mpumalanga Black Aces, Amazulu na Chuo Kikuu cha Pretoria.
Ni kocha anayeheshimika sana kwa mchango wake katika kukuza vipaji vya vijana na ujenzi wa timu zenye nidhamu na mtindo wa kisasa wa kucheza.
Barker anachukua mikoba iliyoachwa wazi na Dimitar Pantev ambaye Simba iliachana naye Desemba 2, 2025 kwa makubaliano ya pande mbili baada ya kufanya vibaya katika mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Mechi hizo ni dhidi ya Petro Atletico ambayo Simba ilifungwa bao 1-0 nyumbani na dhidi ya Stade Malien ambayo Simba ilifungwa mabao 2-1 ugenini.
Baada ya kupoteza mechi hizo, Simba iko mkiani mwa Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mechi ya kwanza kwa Barker kuiongoza Simba kimataifa itakuwa dhidi ya Esperance de Tunis ya Tunisia.
Wakati huohuo, Barker anaondoka Stellenbosch akiiacha timu hiyo nafasi ya 14 katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini kati ya timu 16, ikiwa karibu na eneo hatari la kushuka daraja.
Mkufunzi huyo alijiunga na Stellenbosch mwanzoni mwa msimu wa 2017-2018 na kuiongoza klabu hiyo kutwaa taji lao la kwanza la ndani katika mfumo wa Kombe la Carling Knockout wakati wa muhula wa 2023-2024. Mkataba wake ulitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Kocha huyo anakuwa wa tatu kuifundisha Simba msimu huu baada ya Fadlu Davids na Pantev.