
MSHAMBULIAJI nyota wa Tanzania, Hasnath Ubamba ameendelea kung’ara nchini Misri akikipigania kikosi cha FC Masar Women kuendeleza mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake.
Timu hiyo inayomtumia straika huyo Mtanzania kama silaha yake kuu ya ushambuliaji, kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi moja tu ikiwa nazo 55 dhidi ya wapinzani wao wakubwa Wadi Degla SC Women, hali inayofanya mbio za ubingwa kuwa na presha kubwa kila mechi.
Ikiwa zimebaki mechi 12 kumaliza msimu, kila pointi imekuwa na thamani kwa FC Masar. Uongozi wa pointi moja una maana kwamba sare au kupoteza mechi moja tu kunaweza kubadilisha kabisa ramani ya ubingwa.
Hasnath, ambaye amekuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji, ameonyesha ukomavu mkubwa katika mechi za uamuzi, akifunga mabao muhimu na kutengeneza nafasi zilizoisaidia timu hiyo kuendelea kubaki kileleni.
Kwa mujibu wa takwimu za ligi hiyo, FC Masar imekuwa na safu bora ya ushambuliaji msimu huu, jambo linalochangiwa kwa kiasi kikubwa na mchango wa Hasnath, ambaye ameendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
Timu hiyo hadi sasa imeweka kambani mabao 84 ikiwa katika nafasi ya pili kwa timu zilizotikisa nyavu mara nyingi huku inayoongoza kwa sasa ni Wadi Degla iliyofunga mabao 100.