Tanzania yang’ara masoko njeTanzania yang’ara masoko nje

SERIKALI imesema mauzo ya bidhaa za Tanzania katika Soko la Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) yameongezeka kwa asilimia 40. Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema hadi mwaka 2024 mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko hilo yalifikia Dola za Marekani bilioni 3.9.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kapinga amesema AfCFTA imetoa fursa kubwa kwa Tanzania, hususan kwa vijana kwa kupitia mauzo ya bidhaa za kilimo, uongezaji thamani, viungo, chakula, mavazi na bidhaa za viwandani. Amesisitiza kuwa itawawezesha wananchi kuona na kuchangamkia fursa hizo kwa maendeleo yao na taifa kupitia mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa soko hilo huru la biashara Afrika.

Kapinga amesema kupitia AfCFTA, Tanzania imenufaika na masoko ya Nigeria, Djibout, Morocco, Senegal, Ethiopia na Ghana. Pia, alisema Tanzania imenufaika na soko la Umoja wa Ulaya (EU) kutoka Dola milioni 635 mwaka 2023 hadi milioni 686.3.

Soko la Asia Tanzania limeuza Dola bilioni 2.84 mwaka 2024 kwa uzalishaji wa korosho, pamba na nyama ya mbuzi. Kapinga alisema hali hiyo imetokana na ongezeko la uwekezaji na uboreshaji wa biashara, upanuzi wa viwanda na upanuzi wa masoko ya kikanda na kimataifa.

Kapinga alisema serikali inaandaa mkakati wa mauzo nje ya nchi ambao utekelezaji wake utajumuisha vijana. “Tunataka mojawapo ya kundi linalopaswa kunufaika na fursa za kupata masoko bora ya bidhaa basi liwe kundi la vijana, tutahakikisha mkakati huu unaendelea kuwa jumuishi,” alisema.

Amesema eneo jingine ni katika kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili wajasiriamali na wafanyabiashara wapate huduma kwa urahisi wa kurasimisha na kusajili biashara. Kapinga alisema serikali imeboresha mifumo ya kielektroniki ya usajili wa biashara na utoaji wa leseni kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambapo huduma zote zinatolewa kupitia njia ya mtandao.

“Tumefanikiwa kuunganisha mifumo hii na mifumo ya taasisi nyingine. Mfumo wa usajili wa ORS umeunganishwa na taasisi nyingine 29 za serikali na binafsi kurahisisha upatikanaji wa taarifa zinazotumiwa na taasisi hizo,” alisema. SOMA: “Tafuteni masoko ya nje ,mtajionea wenyewe”

Amesema Serikali imeandaa mikakati, ikiwemo kuendelea kuboresha mifumo ya usajili na utoaji leseni kuongeza ufanisi, mapitio na kutoa maoni kuhusu sheria zinazohusu BRELA ili ziendane na mabadiliko ya kiteknolojia, kampuni kuhuisha taarifa zake za usajili na kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine.

Kapinga amesema kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), vijana wanawezeshwa kupitia mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara na kuwasaidia kufikia masoko ya kikanda na kimataifa. Pia, serikali imeanzisha programu atamizi zinazowalea wajasiriamali na wabunifu na kuwaingiza sokoni kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini (TIRDO) na Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO).

“Lengo letu tunapowakuza, hatutaki waishie palepale na mawazo yao, tunataka tuwaingize kwenye soko waweze kuzalisha, kuuza na kuleta ajira kwa vijana wenzao,” alisema. Kuhusu kusimamia ubora wa viwango chini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), serikali imepanga liwe shirika wezeshi. “Pamoja na majukumu ya kudhibiti ubora na kuwa na nguvu ya udhibiti, tumejipanga TBS iweke nguvu zaidi kwenye kuwa taasisi wezeshi,” alisema Kapinga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *