WAKATI fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 zikitarajiwa kuanza leo Jumapili nchini Morocco, kikosi cha Taifa Stars kitashuka dimbani Desemba 23, 2025 kucheza dhidi ya Nigeria, huku nyota wa zamani wa timu hiyo, Rashid Iddi Chama akisema kila kitu kinawezekana kuanza vizuri.
Taifa Stars iko kundi C pamoja na Tunisia, Uganda na Nigeria na inapewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri kutokana na rekodi za washindani wake.
Chama aliyekuwa na kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki AFCON kwa mara ya kwanza mwaka 1980 nchini Nigeria, aliliambia Mwanaspoti wachezaji wanapaswa kujitambua na kujua wamebeba dhamana kubwa ya taifa la Tanzania.
“Ni kweli kwenye makaratasi tuko kwenye kundi gumu lakini kwenye mpira chochote kinatokea, hakuna kinachoshindikana. Morali tu ya wachezaji inatakiwa kuwa kama wao,” alisema Chama na kuongeza;
“Lakini mimi nina imani wachezaji wetu wakipambana hakuna kitu kinashindikana kwenye mpira, kwa hiyo wacheze kwa moyo mmoja na kwa ari.”
Akidokeza ilivyokuwa mwaka 1980 kwenye AFCON, Chama alisema wachezaji walijijengea utamaduni wa kuhamasishana na kupeana majukumu uwanjani bila kusubiria maelekezo ya kocha, huku akiwataka wachezaji wa Stars kujituma na kujitambua.
Baada ya kucheza dhidi ya Nigeria, Desemba 27, 2025 Taifa Stars itapambana na Uganda kisha Desemba 30, 2025 itamaliza hatua ya makundi ikikabiliana na Tunisia.
Hii ni mara ya nne kwa Taifa Stars kushiriki AFCON ikianza mwaka 1980 nchini Nigeria, kisha 2019 pale Misri na 2023 Ivory Coast na sasa Morocco.
Katika mara zote tatu zilizopita, Taifa Stars haijawahi kuvuka hatua ya makundi wala kupata ushindi wa mechi yoyote, huku mwaka 2019 ikiondoka bila ya pointi wakati 1980 ikikusanya pointi moja na 2023 pointi mbili.