MBEYA; Baraza la Ushindani (FCT) limefanya semina ya elimu kwa wadau kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu majukumu, mamlaka na huduma zinazotolewa na baraza hilo, pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisheria na kidijitali katika usimamizi wa rufaa.
Semina hiyo ilifunguliwa rasmi na Katibu Tawala Msaidizi – Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Mbeya, Anna Mwambene, ambaye aliwahimiza washiriki kutumia ipasavyo mifumo ya kisheria iliyopo katika kutafuta haki na kuwa mabalozi wa kuitangaza huduma za Baraza la Ushindani kwa wadau wengine.
Katika semina hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mbeya,, Baraza la Ushindani liliwapatia washiriki elimu kuhusu matumizi ya mfumo wa kidijitali wa kuwasilisha rufaa zinazotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na mamlaka za udhibiti zikiwemo LATRA, EWURA, TCRA, TCAA na PURA.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Ofisa wa TEAMA kutoka Baraza la Ushindani, Athuman Kanyegezi, ameeleza kuwa mfumo huo wa kidijitali unamwezesha mtumiaji kuanzisha akaunti, kuwasilisha rufaa kwa njia ya mtandao, kupakia nyaraka muhimu, kulipa ada husika na kufuatilia hatua za mwenendo wa kesi bila ulazima wa kufika ofisini, hivyo kuokoa muda na gharama.
Semina hiyo iliwahusisha wafanyabiashara, wajasiriamali pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi, ambapo washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu taratibu za rufaa, matumizi ya mifumo ya kidijitali na upatikanaji wa haki kwa uwazi na ufanisi.