TANZANIA inaungana na mataifa mengine duniani kufurahia Sikukuu ya Krismasi inayoadhimishwa Desemba 25 kilamwaka, siku inayokumbusha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, tukio lenye ujumbe mzito wa upendo, amani na matumaini kwa binadamu wote.
Krismasi ni sikukuu yenye nafasi ya kipekee katika maisha ya waumini wa dini ya Kikristo, lakini pia imeendelea kuwa tukio la kijamii linalokusanya watu wa imani na tamaduni mbalimbali. Ni kipindi ambacho familia hukutana, ndugu na jamaa huimarisha uhusiano, na jamii hujenga mshikamano kwa kusaidiana, hususan kwa wahitaji. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kikristo, kuzaliwa kwa Yesu Kristo kunatoa funzo la unyenyekevu na upendo wa dhati.
Yesu Kristo alizaliwa katika mazingira ya kawaida, akionesha kuwa thamani ya mwanadamu haipimwi kwa mali wala hadhi, bali kwa utu na matendo mema. Ujumbe huu unaendelea kuwa muhimu katika jamii ya sasa inayokabiliwa na changamoto za umaskini, migogoro na mmomonyoko wa maadili.

Wakizungumza na HabariLEO jijini Dar-es Salaam baadhi ya waumini wa dhehebu la Katoliki wanasema Sikukuu ya Krismasi inawakumbusha wakristo wengi kuishi katika matendo mema kwa maisha ya ukristo na kuepuka kufanya dhambi. “Kuzaliwa kwa Yesu Kristo mwanzo wa ukombozi kwa wakristo,” anasema Benard Shija. “Tunaamini kwa kuzaliwa Yesu Kristo sisi tumepona,” anasema muumini mwingine wa dhehebu la Katoliki Rose Shirima.
Katika kipindi cha Krismasi, makanisa mbalimbali huendesha ibada maalumu za shukrani, huku waumini wakihimizwa kuishi kwa misingi ya upendo, uvumilivu na kusameheana. Aidha taasisi na watu binafsi hutumia fursa hii kutoa misaada kwa watoto yatima, wazee na makundi mengine yenye uhitaji, jambo linaloendeleza mshikamano wa kijamii. “Sikukuu ya krismasi inatufundisha pia kukumbuka wengine wanaohitaji msaada kutoa sadaka ni jambo la kiimani,” anasema Meshack Mkomi. SOMA: Makosa ya kifedha katika Krismasi, Mwaka Mpya

Hata hivyo, viongozi wa dini na jamii wamekuwa wakikumbusha wananchi kuepuka matumizi mabaya ya rasilimali na kusherehekea sikukuu hii kwa kuzingatia maadili, amani na usalama. Wito unatolewa kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya heshima na maadili mema, hasa katika kipindi hiki cha sherehe.
“Wakati mwingine watoto wanatakiwa pia kupewa mafunzo ya dini yetu ya kikristo kufahamu umuhimu wa kutambua Sikukuu ya Krismas ambayo ni muhimu katika maisha yao,” anasema Meshack na kuongeza: Aliongezea kuwa, “Lazima wapewe mafunzo ya kufahamu mwokozi wao Yesu Kristo alizaliwa kwa ajili yao.”
Wakristo wengi katika Sikukuu ya Krismasi wanatafakari mwenendo wa maisha na kuweka mikakati mipya ya maendeleo binafsi na ya kitaifa. Ni fursa ya kuimarisha umoja, kudumisha amani na kujenga matumaini mapya kwa mustakabali bora wa jamii na Taifa kwa ujumla. Kadri sherehe za Krismasi zinavyoendelea, jamii inahimizwa kudumisha upendo, mshikamano na kujali wengine, si kwa kipindi cha sikukuu pekee, bali kama sehemu ya maisha ya kila siku.