Katika ujumbe unaofanana uliochapishwa kwenye mtandao wa X, mwakilishi wa Marekani Steve Witkoff na mwenzake wa Ukraine Rustem Umerov wameyataja mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa juma huko Miami kuwa “yenye kujenga” lakini hakuna upande uliotangaza mafanikio yoyote makubwa yaliyopatikana.

Wawakilishi hao pamoja na washirika wa Ukraine barani Ulaya walikuwa Miami tangu Ijumaa iliyopita kwa mazungumzo mapana ya kujaribu kuutafutia suluhu mzozo wa Urusi na Ukraine unaelekea kutimiza miaka minne.

Witkoff na Umerov wamesema sehemu kubwa ya mashauriano ya mara hii yalijikita kwenye uhakika wa usalama na ulinzi wa Ukraine baada ya vita na mpango wa kuujenga upya uchumi wa nchi hiyo.

Tamko lao limesema utawala mjini Kyiv umedhamiria kupata amani ya haki na ya kudumu kwenye mkataba wowote utakaofikiwa ili kumaliza vita.

Zelenskyy asema anasubiri kuhabarishwa yaliyojiri Miami 

Washirika wa Ukraine barani Ulaya walipokutana na Volodymyr Zelenskyy mapema wiki iliyopita mjini Brussels.
Washirika wa Ukraine barani Ulaya walipokutana na Volodymyr Zelenskyy mapema wiki iliyopita mjini Brussels. Picha: Lisi Niesner/AP Photo/picture alliance

Kupitia ujumbe wake wa kila siku kwa taifa, Rais Volodymyr Zelenskyy aligusia mazungumzo hayo yaliyofanyika nchini Marekani na kile kilichokuwa mezani.

“Kazi ya kutayarisha nyaraka za kumaliza vita, uhakika wa usalama na ujenzi mpya (wa Ukraine) inaendelea — wanapitia kila kipengele kwa umakini, na upande wa Marekani umeonesha utayari wa kushiriki kikamilifu. Na hilo ni muhimu. Pia wanajadili – muda mwafaka kwa maamuzi mahsusi. Ninatarajia kupata ripoti ya kina kutoka kwa Rustem Umerov na  Andrii Hnatov kuhusu undani wa mazungumzo hayo.” amesema kiongozi huyo. 

Mazungumzo ya Miami ilikuwa ni mwendelezo wa mashauriano yaliyofanyika mjini Berlin zaidi ya wiki moja iliyopita. Ulaya imekuwa na wasiwasi tangu Marekani ilipochapisha nyaraka yake yenye vipengele 28 vya kumaliza vita na kuishinikiza Ukraine ivikubali haraka iwezekanavyo.

Sehemu yake inahusu kuitaka Ukraine iridhie kuachia maeneo ya ardhi yanayodhibitiwa sasa na Urusi ambayo imeyanyakua baada ya kuanza kwa vita. Hilo ni moja ya suala tete zaidi kwenye mazungumzo yanayoendelea na Ukraine imeonesha upinzani wake mkali.

Urusi yasema imeridhishwa na mazungumzo huku mapigano yakiendelea 

Bandari kwenye jimbo la Krasnodar nchini Urusi.
Bandari kwenye jimbo la Krasnodar nchini Urusi. Picha: Alexander Strela/Zoonar/picture alliance

Kwenye mazungumzo ya Miami, Urusi pia ilimtuma mpatanishi wake mkuu Kirill Dmitriev aliyefanya mazungumzo na wawakilishi wa Marekani bila ya kukutana na wale wa Ukraine.

Siku ya Jumamosi, mwakilishi huyo wa Urusi alisema majadiliano aliyoyafanya na wenzake wa Marekani yalikuwa mazuri.

Wakati mazungumzo yakiendelea, hali kwenye uwanja wa vita bado ni mbaya. Ukraine ilifanya shambulizi la droni usiku wa kuamkia leo kwenye jimbo la Krasnodar, kusini mwa Urusi na kuharibu meli mbili pamoja na maeneo mawili ya kuegesha vyombo vya majini.

Hayo yametangazwa na mamlaka za Urusi ambazo pia zimesema mabaharia wote waliokuwamo kwenye meli hizo wameokolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *