WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema maridhiano ni mchakato unaohitaji uvumilivu, ustahimilivu, unyenyekevu na ushirikiano wa wadau wote. Aidha, amesema maridhiano ni chaguo gumu lakini ni la lazima ili kutibu majeraha kwa nchi. Alisema hayo wakati wa ibada ya ubarikio wa wachungaji na wadiakonia katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe.
Simbachawene amemwakilisha Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kwenye ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Lukajange. Simbachawene alisema katika historia ya dunia, viongozi akiwemo Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Rais wa Kwanza Mwafrika wa Afrika Kusini, Nelson Mandela na Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter waliwahi kusisitiza kwamba maridhiano ya kweli hayafuti yaliyopita bali husaidia taifa kuponya majeraha yake na huanza kwa kusema ukweli na kusikiliza sauti za watu wote.
“Tunapaswa kutambua kuwa maridhiano ya kweli si zoezi la siku moja bali ni mchakato unaohitaji uvumilivu, ustahimilivu, unyenyekevu na ushirikiano wa wadau wote kama serikali, taasisi za dini, taasisi za kiraia na wananchi wote kwa ujumla,” alisema. SOMA: CCM yaja na Tume ya Maridhiano
Ameeleza kuwa kwa niaba ya serikali, ameupokea ushauri na maonyo ya Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk Benson Bagonza kuhusu mambo ya kuepuka katika kufanya maridhiano kama vile kuepuka hila, kukwepa ukweli na kutofanya yasiwe ya kujinufaisha.
“Wajibu wa kujenga taifa lenye amani, umoja, mshikamano na maridhiano ni wajibu wetu sote, viongozi wa maeneo yote serikali, dini na kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha kwamba tunalinda na kudumisha haki, upendo, amani, umoja na mshikamano na kulinda uhuru wa nchi yetu,” alisema.
Vilevile, alisema serikali imeanza na inaendelea kuchukua hatua za kisera zinazolenga kujenga usalama kwa wananchi wote bila ubaguzi, kuimarisha mifumo ya haki na uwajibikaji ili kujenga mazingira ya mazungumzo na maridhiano yanayojenga imani ya wananchi.
Amesema serikali inakubaliana na misingi ya maridhiano, ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume ya kuchunguza matukio ya vurugu siku ya uchaguzi ambayo itatoa ripoti ndani ya miezi mitatu na kuruhusu Watanzania wote kujadili, kushauriana na kujikosoa ili nchi iweze kupona kwa ajili ya ustawi wa kizazi hiki na kijacho.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuthamini uungwaji mkono wa viongozi wa kiroho kama washirika muhimu katika ujenzi wa taifa lenye haki, amani na maridhiano. “Watanzania wote tuendelee kulinda amani yetu, kusema ukweli kwa upendo, kuheshimiana katika tofauti zetu na kushiriki kwa pamoja kujenga Tanzania yenye haki, umoja na matumaini kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.
