Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeonya kuhusu mipango hatari ya Israel dhidi ya Baytul-Muqaddas na kuwafanya Wapalestina kuwa wakimbizi.

Hamas imeelezea uharibifu wa jengo la ghorofa 13 uliofanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Silwan, Baytul-Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu, kama sehemu ya mpango wa kuwafukuza Wapalestina kwa nguvu, na ikatoa onyo dhidi ya mipango hatari ya kudhibiti kikamilifu Baytul-Muqaddas.

Abdul-Rahman Shadid, mmoja wa viongozi waandamizi wa Hamas, amesema: Uharibifu wa jengo la makazi katika mtaa wa Wadi al-Jawz ni mojawapo ya operesheni kubwa zaidi za kuwahamisha kwa kulazimishwa zinazolenga kuwafukuza Wapalestina katika mji wa Baytula-Muqaddas.

 Kiongozi huyo wa Hamas amesema, kitendo hiki ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, na ni kengele ya hatari kuhusu mipango mipana dhidi ya Baytul-Muqaddas.

Abdul-Rahman Shadid amesisitiza kuwa, sera hii ya kivamizi ya utawala wa bandia wa Israel inaendelezwa kwa lengo la kuondoa wakazi wake Wapalestina na kutekeleza miradi ya vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na kuliyahudisha eneo hilo.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitaka jamii ya kimataifa, hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutekeleza majukumu yake na kuchukua hatua za haraka kusitisha vitendo vyote na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina, ardhi yao na maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Madola ya Magharibi yamekuwa yakikosolewa kutokana na himaya na uungaji mkono wao kwa utawala ghasibu wa Israel na hata wengi wanaamini kuwa, himaya hiyo ndiyo inayoupa kiburi utawala huo ghasibu cha kuendeleza uharibifu na jinai zake huko Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *