Ulaya imefadhilisha kutoa misaada yake kwa Ukraine kuliko kutoa misaada hiyo kwa nchi maskini hasa za Afrika.
Kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa bajeti za maendeleo na misaada ya kibinadamu, nchi za Ulaya zimeamua kutoa mhanga mipango ya kupambana na umaskini na njaa barani Afrika na Amerika Kusini, na badala yake kumetanguliza mbele vipaumbele vya kijiografia na kisiasa.
Gazeti la Uingereza la The Guardian limeandika kwamba: Katika miaka ya hivi karibuni, dhana ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya kupambana na umaskini na njaa imepoteza nafasi yake kwa “michezo ya jiografia ya kisiasa” barani Ulaya, huku nchi za bara hilo zikitenga bajeti zao kwa ajili ya Ukraine na gharama za kijeshi.
Nchi za Ulaya zinabadilisha vipaumbele vyao vya kifedha sambamba na kudhoofika na kupunguzwa kiasi kikubwa cha misaada ya Marekani, inayojulikana kama USAID, katika utawala wa pili wa Donald Trump, na programu za afya na kupambana na njaa barani Afrika zimeathiriwa wa mabadiliko haya.
Mwezi huu wa Disemba 2025, Sweden imetangaza kwamba itapunguza bajeti yake ya maendeleo kwa krona bilioni 10 (karibu pauni milioni 800) kwa Msumbiji, Zimbabwe, Liberia na Tanzania barani Afrika, na Bolivia huko Amerika Kusini. Wakati huo huo, bajeti ya misaada ya kibinadamu ya Ujerumani kwa mwaka ujao wa 2026 imetangazwa kuwa euro bilioni 1.05 (£920 milioni), ambayo ni chini ya nusu ya bajeti hiyo mwaka huu 2025, na itazingatia maeneo ambayo yanaangukia kwenye “vipaumbele vya Ulaya”.

Nchi zingine za Ulaya pia zinafuata mkondo huo. Uingereza imepunguza misaada yake ya kibinadamu ili kufadhili gharama za kijeshi, na Norway imeongeza bajeti yake ili kusaidia Ukraine badala ya nchi za Afrika. Ufaransa pia imepunguza bajeti yake ya misaada ya kibinadamu kwa euro milioni 700 na kupunguza msaada wa chakula kwa asilimia 60, huku ikitenga euro bilioni 6.7 kwa masuala ya kijeshi.
Wataalamu wanaonya kwamba maamuzi haya yatadhoofisha mifumo ya kukabiliana na migogoro ya ndani na kuhatarisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni katika sekta za afya ya watoto na elimu katika nchi za Afrika kama vile Msumbiji, Zimbabwe na Tanzania.
Katika miaka ya hivi karibuni, Ulaya imekabiliwa na vita vya Ukraine kama moja ya changamoto zake muhimu zaidi za kiusalama na kisiasa. Tangu mwanzo wa vita hivyo, nchi za Ulaya zilitoa msaada mkubwa na usio na kifani wa kifedha, kijeshi na kisiasa kwa Ukraine. Mabilioni ya euro za misaada ya pesa taslimu, zana za kisasa za kivita na msaada wa kidiplomasia katika majukwaa ya kimataifa, vimeonyesha kwamba Ulaya iko tayari kulipa gharama kubwa ili kuilinda Ukraine. Wakati huo huo, maswali mazito yameibuka juu ya vipaumbele vya Ulaya kuhusu maeneo mengine ya dunia, hasa bara la Afrika; maeneo ambayo yamekuwa yakisumbuliwa na umaskini, vita vya wenyewe kwa wenyewe, magonjwa na migogoro kwa miaka mingi na ambayo hayajapewa kipaumbele. Nchi za Ulaya, hasa madola ya kikoloni kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, zinawajibika zaidi kwa hali hii mbaya kutokana na karne nyingi za ukoloni na unyonyaji wao katika nchi za Afrika.
Nchi za Kiafrika hasa zimekuwa zikikosoa mwelekeo huu wa Ulaya. Nchi hizo zinaamini kwamba Ulaya inatumia sera za kinafiki na kibaguzi katika kukabiliana na mgogoro wa Ukraine. Kwani, wakati mabilioni ya euro yanatengwa kwa ajili ya Ukraine, nchi nyingi maskini bado zinasubiri msaada wa msingi ili kupambana na njaa, uhaba wa dawa na miundombinu muhimu. Hali hii imekuwa sababu ya kaulimbiu za haki za binadamu ambazo zimekuwa zikitolewa na Ulaya kupoteze thamani yake na kuwa chombo cha kisiasa cha kufuatilia maslahi maalumu.

Mgongano huu unaonekana wazi zaidi katika mtazamo wa kimaadili na kisheria. Kwani, kama kweli kuzingatia misaada ya binadamu, katika kalibu ya haki za binadamu, ni kanuni ya ulimwengu mzima, basi hakupaswi kupewa mazingatio katika jiografia maalumu tu. Kupuuzwa nchi maskini huku rasilimali nyingi zikitengwa kwa ajili ya Ukraine kunaonyesha kwamba vigezo vya kibinadamu vinafunikwa na masuala ya kijiografia – kisiasa. Mwelekeo huu utapunguza imani ya kimataifa kwa Ulaya na kuibua mgawanyiko mkubwa kati ya Kaskazini na Kusini mwa dunia.
Kimkakati, sera hii inaweza pia kuwa na matokeo mabaya kwa Ulaya. Kupuuza migogoro ya kibinadamu barani Afrika na wimbi jipya la uhamiaji vitavuruga utulivu wa kisiasa na kustawisha itikadi kali, masuala ambayo yataathiri pia Ulaya. Kwa hivyo, kuipa mazingatio Ukraine peke yake bila kujali mahitaji ya nchi maskini si tu kwamba hakuwezi kutetewa kimaadili, bali pia kutakuwa na madhara kwa Ulaya katika suala la usalama na uchumi.
Hatimaye inatupasa kusema kuwa, kama Ulaya inataka kuendelea kutoa madai ya kutetea maadili ya kibinadamu, lazima ifanye sera zake ziwe na usawa na uadilifu.