Serikali ya Israel inaingia katika kipindi kigumu cha mvutano wa kisiasa na kijamii, huku shinikizo la ndani likiongezeka dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Masuala makuu yanayozua mjadala ni kukataa kuundwa kwa tume huru ya kitaifa kuchunguza mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023, pamoja na uamuzi wa kuifunga Redio ya Jeshi la Israel.

Mashambulizi ya Hamas ya mwaka 2023 yalisababisha vifo vya takribani watu 1,200 nchini Israel na kutekwa kwa zaidi ya watu 250, tukio lililotikisa taifa hilo na kuibua maswali makubwa kuhusu maandalizi ya kiusalama na uwajibikaji wa kisiasa.

Hata hivyo, Netanyahu ameendelea kupuuza wito wa kuundwa kwa tume huru, akisisitiza badala yake kuanzishwa kwa tume ya serikali. Hatua hiyo imeungwa mkono na kamati ya mawaziri baada ya kuidhinisha muswada uliowasilishwa na mbunge wa chama chake cha Likud.

Muswada huo unatarajiwa kupigiwa kura ya awali katika Knesset siku ya Jumatano, jambo linalozidisha mjadala wa kisiasa nchini humo.

Israel Jerusalem 2023 | Benjamin Netanyahu kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri
Waziri Mkuu Netanyahu anasema nchi ya kidemokrasia haihitaji kuw ana redio ya jeshi, lakini wakosoaji wanasema anatumia hoja hiyo kama kisingizio cha kuminya uhuru wa kujieleza.Picha: Abir Sultan/AP Photo/picture alliance

Ukosoaji mkali wa kisheria na kisiasa

Wataalamu wa sheria, vyama vya upinzani na familia za waathiriwa wa mashambulizi ya Oktoba 7 wamekosoa vikali uamuzi huo, wakisema serikali inalenga kukwepa uwajibikaji wa kisiasa na kijeshi.

Wanakosoa kuwa tume ya serikali haina uhuru wa kutosha na haiwezi kutoa majibu huru kuhusu makosa yaliyotokea kabla na wakati wa mashambulizi hayo.

Wakati huo huo, serikali ya Israel imeibua mvutano mwingine baada ya baraza la mawaziri kupitisha uamuzi wa kufunga kituo maaruf cha redio ya jeshi cha Galei Tzahal, maarufu kama Galatz, ifikapo Machi Mosi 2026.

Serikali inasema hatua hiyo inalenga kulinda hadhi ya jeshi kama taasisi isiyoegemea upande wa kisiasa, ikidai kuwa redio ya kijeshi inayorusha matangazo kwa raia si jambo la kawaida katika demokrasia nyingi.

Hoja za serikali na onyo la wapinzani

Akizungumza katika kikao cha baraza la mawaziri, Netanyahu alitetea uamuzi huo akisema kuwepo kwa redio ya jeshi inayorusha matangazo ya kiraia ni hali isiyo ya kawaida.

“Tunafuata pendekezo la Waziri wa Ulinzi la kufuta Galei Tzahal — redio ya kijeshi inayorusha matangazo chini ya uongozi wa jeshi. Ni hali inayopatikana Korea Kaskazini na labda nchi chache sana ambazo hatutaki kuhesabiwa miongoni mwao,” alisema Netanyahu.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema kufungwa kwa Galatz ni sehemu ya mkondo mpana wa kuvidhibiti vyombo vya habari huru nchini Israel, hasa kuelekea mwaka wa uchaguzi.

Kiongozi wa upinzani Yair Lapid ameonya kuwa hatua hiyo inalenga kuondoa sauti za ukosoaji dhidi ya serikali.

“Hii ni sehemu ya mashambulizi ya jumla dhidi ya vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza, hasa katika mwaka wa uchaguzi. Hawataishia kwa Galatz pekee,” alisema Lapid.

 Israel Tel Aviv | Yair Lapid
Kiongozi wa upinzani Yair Lapid ameonya kuwa inachokifanyaserikali ya Netanyahu ni sehemu ya mashambulizi ya jumla dhidi ya vyombo vya habari na uhuru wa kujielezaPicha: Eyal Warshavsky ZUMAPRESS.com/picture alliance /

Ubomoaji Silwan na wasiwasi wa haki za binadamu

Wakati mvutano wa kisiasa ukiendelea, hali ya wasiwasi pia imeshuhudiwa katika eneo la Silwan, Jerusalem Mashariki, ambako tingatinga za Israel zimebomoa jengo la ghorofa nne.

Ubomoaji huo umeacha takribani wakazi 100 wa Kipalestina bila makazi. Wakazi wanasema walilazimishwa kuondoka usiku wa manane na kupewa muda mchache tu wa kuchukua nyaraka muhimu.

Mashirika ya haki za binadamu yameeleza tukio hilo kuwa sehemu ya sera ya kimfumo ya kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka maeneo ya Jerusalem Mashariki.

Kwa upande wake, manispaa ya Jerusalem imesema ubomoaji huo ulitekelezwa kwa mujibu wa amri ya mahakama ya mwaka 2014, ikidai jengo hilo lilijengwa bila kibali.

Hatua hizi zote zinajiri wakati Israel inaelekea katika mwaka wa uchaguzi, chini ya kivuli cha vita vya Gaza, maswali ya uwajibikaji wa kisiasa na hofu inayoongezeka kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini humo.

Wachambuzi wa siasa wanasema miezi ijayo itakuwa ya maamuzi makubwa kwa mwelekeo wa kisiasa wa Israel na nafasi ya uhuru wa kiraia katika taifa hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *