
Wajumbe kutoka Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameafikiana kwamba nchi za Maziwa makuu zinapaswa kuhusishwa katika juhudi za kuutatua mgogoro huo ambao sasa unaihusisha Burundi moja kwa moja.
Mkutano wa dharura kuhusu mgogoro wa mashariki mwa Kongo ulioongozwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni ulimalizika siku ya Jumapili kwenye ikulu ya mjini Entebe.
Wajumbe kutoka mataifa 12 wa nchi wanachama kwenye kongamano la kimataifa kuhusu Kanda ya maziwa makuu walihudhuria mkutano huo ulioitishwa kujadili kwa undani umuhimu wa mataifa hayo ya Afrika kutoachwa nyuma katika kutafuta suluhu kwa mgogoro huo.
Pande zote mbili katika mzozo huo yaani Rwanda na Jamhuri ya Kidemorkasia ya Congo zilizojumuisha maafisa wa ngazi za juu walitoa mapendekezo yao ya kuwezesha kusitishwa kwa vita. Ila kila upande umendelea kulaumu mwingine kwa kutoheshimu mikataba mbalimbali inayolenga kutoa suluhu la kudumu kuhusu mzozo kati yao.
Rwanda inayatuhumu majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi kuwa yamekiuka usitishaji mapigano kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa karibuni huko Washington kwa lengo la kuhitimisha hali ya mchafukoge mashariki mwa Kongo.
Tarehe 4 mwezi huu wa Disemba Marais wa Congo na Rwanda walisaini makubaliano ya amani na uchumi kwa lengo la kuhitimisha mapigano huko mashariki mwa Kongo.
Hata hivyo Rwanda inadai kuwa Kongo imetamka wazi kuwa haitaheshimuusitishaji vita wowote, na kwamba ilikuwa ikipambana kuyatwaa maeneo yaliyoangukia mikononi mwa waasi wa AFC/M23 hata kama mchakato wa amani utaendelea.