Shirila la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Libya lilitangaza jana Jumatatu kuwa limeidhinisha mradi wa dola milioni 5.8 unaofadhiliwa na Kituo cha Mazingira Duniani (GEF) ili kushughulikia changamoto za mazingira na maendeleo katika bonde la Maziwa ya Ubari huko magharibi mwa Libya.

Katika taarifa yake, shirika la Umoja wa Mataifa la UNDP limesema kuwa mpango huo wa miaka mitano, utakaotekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya Mazingira ya Libya, utazingatia kupambana na uharibifu wa ardhi na upotevu wa bayoanuwai sambamba na kusimamia maendeleo endelevu ya kiuchumi katika eneo hilo la jangwani.

Mradi huo pia utaweka msingi wa Hifadhi ya Taifa ya Maziwa ya Ubari kama iliyopendekezwa; na hifadhi hiyo itajumuisha takriban hekta 100,000 za ardhi na kukarabati hekta 225 za ardhi oevu na maziwa ya katikati ya jangwa.

UNDP imesema kuwa mpango huo unatarajiwa kusaidia takriban watu 2,250 – nusu yao wakiwa wanawake – kupitia fursa za ajira endelevu na kuleta karibu nafasi mpya 700 za ajira katika utalii wa ikolojia na kilimo endelevu.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya UNDP imesema: Kuunganisha kazi za utatuzi zinazotegemea maliasili, mila na desturi za kitamaduni za wenyeji wa maeneo hayo ni hatua muhimu kuelekea kutimiza malengo ya maendeleo ya Libya ya kulinda mazingira na hali ya hewa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ueneaji wa Jangwa na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *