HAIKUWA kinyonge. Nigeria wenyewe wameukubali mziki wa Taifa Stars katika mechi ya kwanza ya fainali za mataifa ya Afrika huko Morocco kwa namna ilivyotoa upinzani licha ya kikosi cha Super Eagles kusheheni mastaa wanaocheza soka la kulipwa Ulaya.

Pamoja na Stars kupoteza kwa mabao 2-1, miongoni mwa wachezaji waliokuwa gumzo huko Nigeria ni pamoja na beki wa Yanga, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ aliyekula sahani moja na mshambuliaji hatari, Victor Osimhen anayekipiga Galatasaray ya Uturuki.

Hilo limeelezwa na mwandishi wa habari nchini humo, Samweli Areo aliyesema haikutegemewa kama Osimhen angedhibitiwa kiasi kile kabla ya kufanyiwa mabadiliko katika dakika ya 86 na nafasi yake kuingia Paul Onuachu wa Trabzonspor.

“Wengi tuliamini kwamba itakuwa mechi ya upande mmoja lakini imekuwa tofauti Tanzania imetuonyesha upinzani mkubwa na wengi tumeshangazwa na uwezo wa yule beki jezi namba nne (Bacca),” anasema.

Pamoja na Bacca kula sahani moja na Osimhen haya ni mambo mengine ambayo yametokea katika mechi hiyo.

MPANGO WA GAMONDI

Kocha wa Taifa Stars, aliingia na mpango wa timu kucheza boli na akafanya uchaguzi wa kikosi chenye wachezaji ambao wanaweza kuendana na hilo huku akimtumia zaidi Alphonce Mabula Msanga anayecheza soka la kulipwa nchini Azberjain katika klabu ya Shamakhi kuvuruga mipango ya Nigeria katika eneo la kati alitumika zaidi mbele ya mabeki wa kati.

Gamondi alijua ubora wa Nigeria hivyo kuwa na Mabula kuliisaidia Stars huku Novatus Dismas ambaye hakuanza vizuri mechi katika dakika 45 za kipindi cha kwanza akiwa na jukumu la kuchezesha zaidi timu, jukumu ambalo alilifanya vizuri zaidi kipindi cha pili.

Kwa kutambua urefu wa washambuliaji wa Nigeria, Gamondi alianza na Bakari Nondo Mwamnyeto akicheza sambamba na Bacca, hesabu hizo zilijipa kutokana na kazi kubwa nzuri ambayo ilifanywa na beki huyo ambaye aliokoa mpira ambao Osimhen alimzidi ujanja kipa wa Stars, Zuberi Foba.

Kuwa na wachezaji wenye kasi katika maeneo ya pembeni na katikati mwa uwanja nao ulikuwa mpango mwingine wa Gamondi ambao ulifanya kazi vizuri wakati timu ikishambulia na kuzuia, Charles M’Mombwa mfungaji wa bao la Stars, Simon Msuva, Tarryn Allarakhia wote hao walikuwa wakipanda na kushuka huku juu akisimama nahodha, Mbwana Samatta.

KILICHOIANGUSHA STARS

Mbali na kujisahau kwa wachezaji wa Stars wakati nyota wa Fulham, Alex Iwobi akichonga krosi iliyomaliziwa kwa kichwa na Semi Ajayi, changamoto kubwa ilikuwa namna ya kudili na mipira ambayo Nigeria ilikuwa ikiitupa nyuma ya ukuta wao.

Iwobi na Chukwueze  ndio waliokuwa wakifanya kazi hiyo, walipiga mipira mingi nyuma ya ukuta wa Stars kitu ambacho kilikuwa kikiifanya timu hiyo ya taifa kuwa katika hatari ya kuruhusu mabao, hata hivyo ubora wa Foba wakati akijaribu kupunguza goli ulisaidia.

Pia changamoto nyingine ilikuwa utulivu hasa kipindi cha kwanza, angalau cha pili timu ilitulia na kujaribu kutengeneza nafasi hivyo hili ni eneo ambalo kocha Gamondi anapaswa kulifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi kabla ya kuivaa Uganda, Jumamosi.

Hata kukosekana kwa kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi ya njano, kuliinyima Stars nafasi ya kutengeneza nafasi kwa vile viungo Mabula na Dismas wote kuwa wakabaji na kushindwa kuifanya timu itembee mbele.

Mechi ijayo wikiendi hii, Fei Toto anatarajiwa kurejea uwanjani kukabiliana na Uganda ‘The Cranes’ ambayo nayo ilianza kwa kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Tunisia.

MABADILIKO YA MBINU

Baada ya kuanza na mfumo wa 4-3-3, Gamondi aliamua kubadilika kimbinu kufuatia kuwa nyuma kwa mabao 2-1, kuanzia dakika ya 79 baada ya kufanya mabadiliko mawili kwa mpigo, aliwatoa Shomary Kapombe na Allarakhia huku wakiingia Haji Mnoga na Dickson Job.

Mabadiliko hayo yaliifanya Stars kuwa na mabeki watatu wa kati yani Job, Bacca na Mwamnyeto huku Haji na Mohammed Hussein wakipanda zaidi kuongeza nguvu ya mshambulizi ili kutafuta bao la kusawazisha hivyo Stars ikawa na idadi kubwa ya wachezaji mbele.

Wakati ambao timu ilikuwa ikishambuliwa mabeki hao wa pembeni walirudi kwa haraka na kuongeza namba ya mabeki kuwa watano, ndani ya dakika hizo chache zilizosalia Stars ilitengeneza nafasi kadhaa ambazo hata hivyo ilishindwa kuzitumia.

M’MOMBWA ACHEKELEA REKODI

Licha ya bao lililofungwa na M’Mombwa kutoisaidia Stars dhidi ya Nigeria limeweka rekodi kuwa goli la kwanza kutoka kwa mchezaji anayecheza ligi ya Malta kufungwa katika AFCON.

Yani kama hukuelewa iko hivi; haijawahi kutokea mchezaji yeyote aliyewahi kucheza ligi hiyo kabla ya M’Mombwa na akafunga bao katika AFCON na yeye ndo kaweka nyavuni kuvunja mwiko.

“Nilifunga wakati sahihi ambao tulikuwa tukipambana kurudi mchezoni, niliamini kuwa tunaweza kupata zaidi lakini haikuwa bahati yetu ila bado nafasi tunayo katika mechi zilizosalia kufanya kitu tofauti,” anasema nyota huyo wa Floriana.

MSIKIE GAMONDI

“Tulicheza dhidi ya timu yenye ubora mkubwa na uzoefu wa hali ya juu, lakini hatukuwa waoga. Tulionyesha nidhamu ya kiufundi, ushindani na ujasiri hadi dakika ya mwisho,” anasema Gamondi.

Anaongeza kuwa makosa madogo ndiyo yaliigharimu timu:

“Katika mechi za kiwango hiki, kosa moja au mawili yanaweza kukuadhibu. Tuliruhusu mabao kwa nyakati ambazo tulipaswa kuwa makini zaidi, lakini pia tuliweza kutengeneza nafasi na kufunga goli muhimu.”

“Hili ni kundi gumu, lakini bado tuna mechi nyingine mbele yetu (dhidi ya Uganda). Tunaenda kufanyia kazi upungufu uliojitokeza ili kuwa bora zaidi katika mechi inayofuata.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *