
Algeria. Bunge la Algeria limepitisha sheria inayotangaza ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria kuwa ni uhalifu.
Wabunge wa Algeria walipokutana bungeni Jumatano, walifungua kikao kwa kuimba wimbo wa taifa.
Baadaye walipitisha kwa kauli moja muswada unaotangaza ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria kuwa ni uhalifu wa dola.
Sheria hiyo mpya inaitaka Ufaransa kuomba radhi na kutoa fidia.
Rais wa Bunge alisema muswada huo unatuma ujumbe wa wazi wa kisiasa kwamba kumbukumbu ya Algeria haiwezi kufutwa wala kujadiliwa.
Ufaransa ilitawala taifa hilo la Afrika Kaskazini kuanzia mwaka 1830 hadi 1962. Vita vya umwagaji damu vya kudai uhuru vilivyodumu kwa miaka minane viliua mamia ya maelfu ya raia wa Algeria.
Sheria hiyo inaorodhesha makosa mbalimbali yaliyotekelezwa na wakoloni wa Kifaransa, yakiwemo mateso, majaribio ya silaha za nyuklia na uporaji wa rasilimali.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, hapo awali alikiri kuwa ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria ulikuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, lakini hakufikia hatua ya kuomba radhi rasmi.
Muswada huo hauna nguvu ya kisheria kwa Ufaransa, lakini wachambuzi wanasema unaashiria mpasuko mkubwa katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kuzorota kwa mahusiano
Mvutano kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukiendelea kwa miezi kadhaa, ukichochewa zaidi na uungaji mkono wa Ufaransa kwa mpango wa Morocco wa kutoa uhuru wa ndani kwa eneo lenye mgogoro la Sahara Magharibi msimamo ambao Algeria inauona kama usaliti wa msimamo wake wa muda mrefu wa kuunga mkono haki ya watu wa Sahara (Wasahrawi) ya kujitawala.
Pia, hivi karibuni nchi hizo zimejihusisha katika kufukuziana wanadiplomasia, kufuatia kukamatwa kwa afisa wa ubalozi wa Algeria nchini Ufaransa.
Masuala ya uhamiaji nayo yamekuwa chanzo cha mvutano. Ufaransa imeituhumu Algeria kwa kukataa kuwapokea tena raia wake waliotimuliwa kutoka Ufaransa, jambo lililoisukuma Ufaransa kuweka vikwazo vya usafiri kwa wamiliki wa pasipoti za kidiplomasia za Algeria.
Algeria ililaani hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa makubaliano ya pande mbili na ikaonya kuhusu kuchukua hatua kali na za haraka za kulipiza kisasi.